PIERRE LIQUID; Pampula 'flani' hivi amazing

TANZANIA ipo juu, ipo kileleni. Hiyoooo! Itabaki kileleni. Nchi inazidi kutisha kwa kuongoza mwendo. Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ndiye ‘genius’ wa siasa Afrika kuwahi kutokea na atabaki kileleni. Hutaki nivizie barabarani na mayai viza!

Diamond Platnumz, Ali Kiba, Harmonize na wengine kibao ni funika bovu Afrika Mashariki. Majanki wameifanya Tanzania iwe makao makuu ya muziki ukanda wa Afrika Mashariki na Kati. Ikibidi chukua eneo lote la maziwa makuu. Ukibisha jichome msumari wa koo!

Simba ndiyo mabingwa wa kihistoria Kombe la Afrika Mashariki na Kati. Hapa hatubishani, rekodi ndiyo zinanena kwa herufi kubwa. Tena, Simba ndiyo klabu pekee Afrika Mashariki ambayo imefuzu robo fainali ya Klabu Bingwa Afrika. Usininunie mimi. Wanunie Caf!

Simba na Yanga ndiyo derby yenye nguvu Afrika Mashariki na Kati na ina msisimko mkubwa kuliko derby zote Afrika. Utaniambia nini? Tanzania ipo kileleni. Inaongoza siasa, burudani, michezo.

Hata sasa, Tanzania inang’ara kwa ulevi. Juzikati watumishi wa Mungu Rombo, Kilimanjaro, walianza ibada maalum ya funga ili kuwaombea wakazi wa wilaya hiyo ambao wamekithiri kwa ulevi. Kuna kipindi wanawake Rombo walikwenda Kenya kuomba hifadhi ya wanaume, sababu waume zao wanautwika mpaka wanasahau majukumu yao muhimu nyumbani.

Sema nini, wale wanawake wa Rombo miyeyusho sana. Tanzania wanaume wamejaa tele. Wengine huwanyatia mpaka wanawake wenye ugonjwa wa akili na kuwajaza ujauzito. Badala ya kutangaza njaa zao Tanzania humuhumu wasaidiwe, wao wakaenda nchi jirani. Kusudi ionekane wanaume wa Tanzania si wachangamfu. Wanawake wa Rombo siyo wazalendo.

Muulize RC wa Dar, aliita wanawake waliotelekezewa watoto wajitokeze. Walijaa kibao! Unaambiwa waliojitokeza ni sehemu ndogo sana. Wengi waliuchuna kwa aibu ya kamera za wanahabari. Hiyo ilikuwa alama yenye kuonyesha wanaume wa Tanzania si goigoi kihivyo lakini tatizo lao hawahudumii watoto. Hivyo wale wa Rombo wasingekosa msaada Bongoland.

Ukweli Tanzania ipo juu. Ipo kileleni. Na sasa tuna ingizo jipya la supastaa. Ni Pierre Liquid, au andika tu Pierre Likwidi. Huyu ni pampula wa Kitaifa. Anaweza kuwa mwanamume pekee duniani ambaye anahimizwa kunywa pombe ili atengeneze pesa.

Pierre anasema mpenzi wake ni pombe. Ukweli niwajuavyo baadhi ya wadada wanaweza kumtengeneza kwa maneno “Pierre nakupenda jinsi unavyokata ulabu.” Si unajua sasa hivi pesa ya kubadili mboga haikosekani? Au girlfriend wake hashindwi kumwambia “Baby nenda kalewe tupate pesa. I love you chapombe wangu.”

Ukiacha waonja pombe wa viwandani, Pierre anaweza kuwa binadamu pekee ambaye anaingiza pesa kwa kukaa baa na kunywa. Amekuwa kivutio Tanzania, kisha amevuka mipaka. Vyombo vya habari Kenya, vikajichanganya kwa kumtangaza ni msanii wa kitaifa kutoka Tanzania. Wakakosolewa, wakaambiwa yule ni mlevi wa kitaifa. Sokomoko wa kitaifa a.k.a pampula wa kitaifa.

Pamoja na hivyo, huo ndiyo ukweli, Pierre ni mlevi amazing. Amegeuka kivutio. Mabaa yanamlipa pesa ili akalewe, kisha wanatangaza “Pierre atakuwepo hapa”. Naam, watu nao wakisikia Pierre atakuwepo wanajaa kwa wingi. Wanapenda mambo ya Pierre anapokuwa amejitwika bruarizi za kutosha kichwani.

Hiyo ikawa sababu ya Kenya kumpa dili akawe kivutio na kwao. Yes, kama wanamuziki wetu wanavyokwenda nchi nyingine kupiga shoo na kutengeneza mabovu, ndivyo na Pierre alivyokwenda Kenya kugonga shoo ya ulevi na kukusanya noti. Kama utani, Pierre anakuwa mlevi milionea. Pampula ‘flani’ amazing ambaye ameamua kuugeuza ulevi kuwa fursa ya kifedha.

Shoo yenyewe anapiga basi? Ni zile mbwembwe na vituko vyake akiwa amelewa, ndivyo huwaacha watu hoi. Mara alie, mara acheke. Asifie kwa maneno yake “utabaki kileleni” na kamsemo kake ka “aai mama nakufa”, utawaambia nini watu kwa Pierre? Riziki haiandikiwi barua.Huja vyovyote.

Pierre imemkuta baa akifanya vituko baada ya kulewa. Mwite Mlevi The Don.

Katika wimbo Tetema wa Rayvanny ft Diamond, Rayvanny anasikika akirejea vimisemo vya Pierre “aai mama shigidi aah, nakufa hoi wikidi aah, aai mama shikidi konki, faya moto likwidi.” Maneno yake ni yaleyale tu. Koki faya, hatari faya. Utabaki kileleni. Mdogomdogo anatoboa na sasa yupo kileleni.

Kuna wakati alisema hulipwa Sh1.5 milioni kwa kila mwaliko wa baa. Unaweza kushangaa. Juzi katambulisha gari lake mpya, Toyota Crown. Rangi nyeusi. Mtu mzima amenunua gari kwa sababu analewa. Analipwa fedha sababu analewa. Analewa bure sababu analewa.

DON’T TRY

WWE wana tangazo lao la mieleka linalosema “Don’t try this at home”. Mapambano yao ni burudani na watu wanalipwa fedha. Usije kuona John Cena na The Rocky wanavyorukiana, ukataka nawe umrukie wa kwako nyumbani, utafungwa ukiua au ataumia. Zaidi, unaweza kufa.

Hata hili la Pierre ni don’t try. Pombe inabaki kuwa na matokeo yaleyale unywaji kupita kiasi ni hatari kwa afya yako. Vilevile unywaji sana wa pombe ni hatari kwa uchumi wako. Maana unatumia fedha kununua. Pombe hunyonya fedha. Pombe zina kawaida ya kupunguza ufanisi.

Usije kujidanganya Pierre anatoboa, kwa hiyo nawe uanze kulala baa ukadhani utapiga hela.

Utaishia kuwa kituko tu. Narudia, pombe zina matokeo yaleyale ya siku zote. Pierre anatoboa kwa sababu ni mlevi mwenye bahati. Walevi wote hupuuzwa na vituko vya baa, lakini Pierre amepiga bao. Bahati ya mwenzio usiilalie mlango wazi.

Kwa Pierre pia, cha kufanya ni kutambua kuwa amebahatika. Huu ni wakati wake wa kupiga hela. Kama anavyoitwa kwenye mabaa, vilevile dili za matangazo zitamfuata.

Akumbuke yeye siyo msanii wa vichekesho, bali ni mlevi tu mwenye vituko. Ipo siku atazoeleka na ataonekana hana jipya. Vituko vyake havitakuwa dili.

Hivyo, sasa hivi Pierre apige hela huku akikumbuka kwamba kesho anaweza asipate mchongo wowote.

Ni wakati wake wa kufanya mambo ya maana. Yeye ni mtu mzima, uzuri ana akili timamu. Kwa hiyo, anajua kipi cha kufanya. Pamoja na kila kitu tukubali; Pierre ni mlevi amazing. Ni pampula milionea.