Pascal Cassian afanyiwa upasuaji wa njia ya mkojo

Tuesday March 26 2019

 

By Nasra Abdallah, Mwananchi [email protected]

Hatimaye msanii wa muziki wa injili, Pascal Cassian, amefanyiwa upasuaji nchini India, alikoenda Machi 21, mwaka huu.

Mkali wa kughani mashairi, Mrisho Mpoto aliyekuwa akiratibu safari ya matibabu ya Cassian kwa kushirikiana na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, ameiambia Mwananchi kuwa Machi 22, 2019, Cassian alifanyiwa upasuaji huo na hali yake inaendelea vizuri.

Cassian ambaye ni mshindi wa Bongo Star Search (BSS) 2009, ameugua kwa muda sasa baada ya kupata ajali Oktoba mwaka jana, mkoani Singida, akitokea Kigoma katika shughuli zake za kuhubiri injili. Ajali hiyo ilimsababishia kupasuka kibofu cha mkojo.

Tangu augue amekuwa akiomba msaada kwa watu mbalimbali bila ya mafanikio mpaka Februari 19, mwaka huu, pale Makonda alipojitolea kugharamia matibabu hayo baada ya kuombwa na Mpoto kufanya hivyo.

Katika msaada huo, Makonda aliagiza Cassian apelekwe kwanza Hospitali ya Taifa Muhimbili ambako mbali na kupatiwa vipimo upya, pia iwe rahisi kwa yeye kupata rufaa ya kwenda India, ambapo alikaa hospitalini hapo kwa takribani mwezi mmoja.

Akielezea maendeleo yake, Mpoto alisema wanashukuru hali yake inaendelea vizuri akiwa chini ya uangalizi wa madaktari.

Akielezea kwa undani upasuaji aliofanyiwa msanii huyo, Mpoto alisema amerudishiwa njia yake ya kujisaidia haja ndogo tofauti na awali ambapo walimtoboa sehemu nyingine kwa ajili ya kufanya hivyo.

“Ni jambo la kushukuru baada ya upasuaji huo kwa sasa anaweza kujisaidia kwa njia ya kawaida ambapo kuna kifaa maalumu wamekifunga ambacho atakaa nacho kwa mwezi mmoja.

“Hata hivyo, ile njia mbadala haijafungwa kabisa imeachwa kwa ajili ya dharura na atarejea nchini akiwa anazo zote na baada ya mwezi mmoja madaktari wa hapa nchini watamtoa na kurudi katika hali yake ya kawaida,” alisema Mpoto.

Advertisement