Ndani ya Boksi: Siyo Mondi, Konde Boy peke yao wanaoigana

Unaweza kusikia watu wanalalamika eti oooh wasanii wakubwa wanaiga, tena wengine wanawataja hadi Mondi na Konde Boy lakini heu tujiulize, nyinyi watangazaji wa redio na runinga, hivi nani aliwaambia saa mbili usiku ndiyo muda sahihi uliobarikiwa kwa taarifa ya habari? Hivi ni nani aliwaambia asubuhi kila redio iwe na kipindi kama ‘cha mazungumzo na kubishana kama vinavyofanywa na redio nyingi hapa nchini’?

Sawa lakini si kila kitu mfanane. Mnaweza wote mkawa mnachambua habari za magazetini lakini ikawa tofauti kidogo. Kila redio inachambua magazeti kwa mtindo na mtiririko ule ule.

Ingefaa wakati mwingine kuwaita hata wahariri wa magazeti ili wachambue na kujitofautisha kidogo. Redio na runinga karibu zote zina vipindi vilivyo katika maudhui sawa. Inachefua kidogo.

Hao wa vipindi vya mchana redioni ndiyo wanaigana mpaka namna ya kutamka maneno. Kuna wakati hadi usubiri ‘jingo’ ya jina la redio ndipo ujue unaisikiliza ipi. Kwa sababu ya kufanana sauti na matamshi kwa watangazaji. Sauti namna ya kutamka maneno mpaka utani kwenye vipindi ni ule ule. Na majina ya a.k.a kila mtangazaji. Badilikeni aisee mnachosha sana. Sawa usiku ni muda mzuri kwa vipindi vya mahaba lakini ndiyo kila kipindi kiongelee ngono tu?

Kuna mambo mengi ya kuzungumzia juu ya uhusiano lakini watangazaji wengi wa vipindi vya usiku wanaongelea ngono tu badala ya uhusiano. Kwani haiwezekani kuongelea ndoa kwa maana ya ndoa? Kwani kukamata wasikilizaji ni kuongelea ngono tu? Badilikeni.

Mnalaumu Bongo Movie kuigiza mambo ya mapenzi tu huku nyinyi mkitangaza ngono tu muda wote. Hata vipindi vya kina mama ambavyo mara nyingi vipo nyakati zile za kuelekea kwenye mapishi ya mchana ni yale yale kila siku kila redio.

Bongo Movie wakati fulani walikuwa wakiigana sana. Wapo walioiga Wanaijeria na wale walioiga wanaoiga Wanaijeria. Kila muvi ilikuwa lazima awepo mganga wa kienyeji. Halafu kila mganga kajipaka masizi usoni na kuvaa golore jekundu. Mlinzi mwenye akili mbovu na mawenge mawenge.

Na staa yaani mhusika mkuu ni lazima avae suti. Awe na sigara kubwa mdomoni na nywele zenye ‘blaki’. Huu ulikuwa ni utaratibu wa kila muvi. Watengenezaji wa filamu waliamini majengo ya kifahari, magari ya thamani, sauti na kuongea kwa kuchanganya Kiingereza ndo filamu nzuri.

Kila msanii aliamini kwamba filamu Bora ni kuwa na ‘taito’ la Kiingereza. Ukiangalia stori na mazingira ya filamu husika hayaendani kabisa na matumizi ya jina la Kiingereza kwenye ‘kava’. Lakini waliamua kuigana tu bila kueleweka sababu.

Baadaye wakaanza utaratibu wa kutoa filamu yenye mwendelezo yaani part one na two. Akianza mmoja kufanya kitu wanafuata wote. Ilikuwa ukitazama Bongo Movie kama hujawahi kufika Tanzania ungeamini kuwa ni nchi ya kitajiri sana.

Watu waliponda sana na miongoni mwa wapondaji ni watangazaji wa redio na runinga ambao nao wanaigana hovyo.

Wabongo tuna tatizo la ubunifu kwenye mambo mengi. Hii Leo wasikilize wachezaji na makocha wa mpira wakihojiwa. Wote wanaanza na “Kwanza tunamshukuru Mungu tumemaliza mechi salama.” Mwanzilishi wa hii staili ni Cannavaro, leo hii kila mchezaji mpaka kwenye mechi za mitaani.

Ndiyo maana unaona Wabongo hivi sasa wako ‘bize’ kukomenti kwenye kurasa za mitandaoni. Badala ya kupiga simu kwenye vipindi kama enzi za kina Manka Mushi. Mambo ya redioni na runingani ni yale yale kama kulwa na doto, hakuna ubunifu.

Eneo pekee ambalo lina ubunifu mkubwa ni comments mitandaoni. Utacheka ufe kwa maneno ya Wabongo. Nenda kwenye ukurasa wa timu ya Samatta utaelewa ninachosema. Lakini mengine mengi tunaigana sana.

Sikiliza vipindi vya jioni kuanzia saa kumi. Ni yale yale kila redio, hakuna jipya. Na kinachoumiza siku hizi hakuna mtangazaji wa pekee kama enzi za kina Masako, Charles Hilary na Nyaisanga. Wa Sasa wote wanafanana mpaka jinsi ya kuhema kwenye maiki.

Hata wachambuzi wa michezo nao ndo walewale. Kila redio wanachambua kwa kuigana tu mpaka namna ya kutamka maneno. Mtu yuko Tanzania lakini Barcelona anataka kuitamka kama Mgiriki eti Bathelona.

Unaiga mpaka ‘aksenti’ ya Kigiriki. Mtangazaji mwingine kwenye redio nyingine naye anamuiga anayeiga sehemu nyingine. Arsene Wenger anatajwa jina lake na Mswahili wa Mwananyamala Kisiwani eti ‘Asene Venga’.

Anaiga matamshi ya watu wa taifa lingine halafu anatokea mwingine wa Vingunguti naye anamuiga anayeiga sehemu. Badilikeni watangazaji, runinga na redio zinazoacha kufanya ubunifu wa vipindi na maudhui na kuishia kuigana igana kama Nyumbu wa Serengeti.

Any way yawezekana ni utaratibu wa Kitanzania hivi sasa kuiganaigana tu. Maana hata mitandao ya simu nayo kila siku wanaigana kwenye virushi vyao. Kila mtandao unaiga kifurushi cha mtandao mwingine. Yaani promosheni zao zinatofautiana kwa jina la kampuni husika tu.

Zamani wanamuziki wa Bongofleva waliigana kwa vitu vingi. Kila aliyetoa albamu angenunua gari aina ya balloon. Kama alikuwa anakaa maeneo mengine lazima angehamia Sinza. Kuishi Sinza ilikuwa ndoto ya wasanii wengi.

Kuigana kwao ndiko kulikopeleka wengineo waige mpaka matumizi ya unga. Wengine wakapotea kwa kuendekeza ulevi na kukesha kwenye mabaa kama sungusungu. Yote ni kutokana na kuigana mpaka kwenye namna ya kuishi.

Vijana’ wanaigana mpaka ‘fasheni’ kutangulia mbele za haki. Yaani ile ‘kuresti ini pisi’ hata kabla ya wazazi. Na hii ni kwa sababu moja ambayo wengi wetu hatujui kama ni chanzo. Vijana tunaishi kama wazee na wazee wanaishi kama vijana. Ndio maana tunatangulia kabla ya wazee.

Kijana asubuhi tu koo limekauka unawaza baa badala kwenda ‘jimu’ au viwanja vya wazi ukimbie kupunguza futa na nyama uzembe. Kutwa nzima kazi nzito kwako ni kusoma meseji za ‘magrupu’ kibao ya ‘wasapu’ au ‘kufowadi’ ‘meseji’ ‘grupu’ hili kwenda lile. Na kazi ngumu kwako ni kutafuta chaji ya ‘simu janja’.

Unalala saa 8 usiku na vyakula vingi tumboni. Unaamka asubuhi unaoga na kukaa kwenye gari kwenda ofisini. Ukifika ofisini unakaa. Saa nne ukinywa chai unakaa. Mchana ‘lanchi’ hivyo hivyo. Unajaza tu vyakula tumboni bila kazi ngumu, hadi mchana kazi ngumu uliyofanya ofisini ni ubishani wa Mondi na Kiba.

Jioni huyo kwenye gari umekaa tena na foleni za Dar unafikia baa na kamba ya kitambulisho cha kazi shingoni. Kabla ya kuagiza pombe na michemsho unaulizia sehemu ya kuchajia simu. Baada ya hapo ni mtungi na nyama nyama unapakia tumboni. Mpaka minyoo inakerwa kwa kuvimbiwa vyakula vya baa kila siku.

Unarudi ‘homu’ usiku wa manane. Kama uko na manzi unajitumikisha kwake kizushi kisha unalala fofofo. Kesho tena unaamka na ratiba ni ileile mpaka mwisho wa wiki. Mwili hausumbuliwi na lolote labda kuoga na kupaka mafuta. Kama siyo kufunga kamba za viatu utaacha kuvimbiana kama puto?

Mwisho wa wiki muda wote kijana umekaa kibwegebwege tu unakula na kunywa mipombe. Huna na hujui mpangilio wa chakula zaidi ya kumechisha tisheti na simpo. Ndo unachofahamu huna muda wa kutembea hata nusu kilometa kwa wiki mara moja tu.

Sasa uwezo wa kazi za usiku kwa mkeo au bibi wa mtaani unapungua. Unaanza kupoteza pesa kwa vumbi la Kongo. Mwisho unagundua figo mbovu, maini ‘skrepa’, mapafu ‘mkangafu’. Kisukari mara kongosho limekaa kama ‘bedifodi’ ya kijiji. Lazima ‘uresti in pisi’ kabla ya ‘Maza’ na dingilai. Maisha ya kuigana.