AY: Nililala kwenye kontena nikisaka maisha Dar

Sunday January 6 2019

 

By Nasra Abdallah, Mwananchi

Dar es Salaam. Msanii Ambwene Yesaya ’AY’ kwa mara ya kwanza ameonyesha kontena alilokuwa akitumia kulala alipofika jijini Dar es Salaam kutafuta maisha akitokea mkoani Morogoro.

Katika ukurasa wake wa Instagram leo Jumapili Januari 6, 2019 alipiga picha mbele ya kontena hilo lililopo Upanga karibu na klabu maarufu ya zamani ya muziki iliyoitwa California Dreamer.

Picha hiyo ya AY ambaye amesimama mbele ya kontena hilo, imeambatana na maneno akisema “Heri ya mwaka mpya ndugu zangu. Leo ngoja niwaambieni stori kwa ufupi jinsi Ambwene baadaye akawa AY alivyokuja kupambana na maisha Jijini Dar Es Salaam.”

“Nilikuja Dar mwaka 1999 kutoka nyumbani Morogoro kwa msukumo wa ndugu yangu @gzingalize ambaye tulikuwa tunasoma wote Ifunda Technical School Iringa.”

“Nilikuja Dar nikiwa na ndoto moja tu ya kufanikiwa kupitia kipaji changu cha muziki. Nilipofika sehemu niliyoanza kuishi ni kwenye Container hili hapo nyuma, lipo Upanga baada ya mataa ya California Dreamer kama unaenda mjini,” anaeleza.

“Ndio sehemu nilikaa kwa kipindi kirefu kabla sijapewa hifadhi kwa familia ya @gzingalize halafu nikahamia kwa kina @kingcrazy_gk,” amesema AY.

Alieleza Container hilo lilikuwa linatumiwa na mafundi wa kushona nguo hivyo kila siku ilikuwa ni lazima amke saa 12:00 asubuhi kabla mafundi hawajafika.

Pia katika kuoga ilibidi kutembea mpaka Mnazi Mmoja kwenye mabafu ya Jumuiya ambayo ni ya kulipia.

“Mwisho wa siku ilikuwa lazima ndoto itimie bila kujali mazingira husika. Ni muhimu kushukuru kwa kila jambo Mungu analokubariki nalo na kuweka bidii kwenye ndoto zako, period!!.,”aliandika AY.

Historia hiyo inawagusa watu mbalimbali akiwemo msanii Farid Kubanda'Fid q' ambaye anamshauri AY kununua kontena hilo na kulifanya studio na kijiwe cha wasanii wanaotoka mikoani kwenda Dar kuendeleza  harakati zao za sanaa.

Naye barakahtheprince_alichangia ujumbe huo akisema, “Daah bro hii kitu imenipa imani na nguvu sana Mungu wa maajabu alitenda maajabu, hongera sana bro mfano mzuri kwa vijana wapambanaji.”

Advertisement