VIDEO: Ali Kiba aeleza sababu kupanda, kushuka wimbo Dodo Youtube

Muktasari:

Mfalme wa Bongofleva Ali Kiba amesema nyimbo zinapungua idadi ya watizamaji Youtube kutokana na kuripotiwa kuwa zina maudhui ya kuudhi, hivyo kushushwa kwa ajili ya kufanyiwa uhakiki.

Dar es Salaam.  Msanii wa Tanzania, Ali Kiba amezungumzia sababu watazamaji wa wimbo wake wa Dodo katika mtandao wa Youtube kupanda na kushuka akibainisha kuwa kuna mchezo unafanywa na wasioitakia mema tasnia ya muziki nchini.

Wimbo huo ambao Ali Kiba amemtumia  mwanamitindo, Hamisa Mobetto kama mpamba video uliachiwa Youtube juzi Jumatano Aprili 8, 2020 na kutazamwa na watu milioni moja ndani ya saa 24 lakini jana jioni walionekana kushuka na kufikia 750,000 kitu ambacho kiliibua hali ya sintofahamu.

Hata hivyo, leo Ijumaa Aprili 10, 2020 idadi ya walioutazama wimbo huo inaonekana  ni zaidi ya milioni moja.

Akizungumza na Mwananchi leo, Ali Kiba amesema, “kinachotokea ni kuwa mimi au msanii mwingine anapotoa wimbo au  nyimbo kuna watu wanatoa taarifa za uongo Youtube kuwa wimbo husika umetoka kimakosa, una matusi au maneno ya kuudhi.”

“Ikishatolewa taarifa kuhusu hilo,  Youtube lazima waushushe wimbo ili kufanyia uhakiki taarifa zilizoripotiwa, ndiyo maana kuna nyimbo huwa zinapanda katika mtandao huo na kushuka kisha kupandishwa tena.”

Kiba amefafanua kuwa kuna watu wana wataalamu wao wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), wanazivuruga akaunti za mitandao ya watu, akidai kuwa wanafanya hata katika kushusha watazamaji wa wimbo, au kitu kinachowekwa mtandaoni.

“Wapo wanaojisifia katika mitandao ya kijamii kutokana na hizo tabia za kuchezea watazamaji katika mtandao huo,” amesisitiza.

Amebainisha kuwa wimbo na muziki mzuri utabaki kuwa hivyo, “kibaya ni kwa watu wanaochezea mitandao kujiongezea idadi ya watu waliotazama nyimbo zao. Wanajidanganya wao wenyewe ilihali ukweli wanaujua, lakini wanawakatisha watu tamaa wanaondoa morali ya kufanya kazi, wanaondoa ushindani halisi wa muziki.”

Ali Kiba ambaye amewahi kufanya kazi na mwanamuziki wa Marekani, R Kelly amesema, “muziki ni kazi  kwa maana hiyo kila anayeufanya anahitaji kupata ujira,  hivi wanavyofanya wanasababisha watu wasilipwe kulingana na kazi wanayoifanya.”

“Ina maana kuna watu wanaacha kuimba au hawafanikiwi siyo kama hawajui, bali soko linakatisha tamaa kutokana na kuwapo watu wenye tabia za ajabu.”