Aliyeng’ara tuzo za Grammy, ang’ara tena za Oscar

Muktasari:

Mtayarishaji wa muziki, Ludwig Goransson, ameng’ara tena katika tuzo za Oscar, ikiwa ni siku 14 zimepita tangu atwae tuzo za Grammy.

Mtayarishaji muziki, Ludwig Goransson ameshinda tuzo za Oscar ikiwa ni wiki mbili zimepita tangu aliposhinda tuzo za Grammy.

Katika tuzo hizo za Grammy, Goransson ameshinda kama mtayarishaji bora kupitia wimbo wa ‘This is America’ ulioimbwa na Childish Gambino, wimbo ambao pia ndio ulitwaa tuzo ya wimbo bora katika tuzo hizo zinazoheshimika duniani.

Goransson ambaye ana miaka 34, ameonekana kung’ara tena katika tuzo za Oscar zilizofanyika usiku wa kuamkia leo Jumatatu Februari 25, 2019 katika Jimbo la Los Angeles nchini Marekani.

Mtayarishaji huyo alitangazwa kushinda kipengele cha muziki asili uliotungwa kwa ajili ya filamu maarufu ya Blank Panther.

Hata hivyo, hii ni mara ya kwanza kwa Oscar kutangaza kipengele hicho cha muziki asili na Goransson kuwa wa kwanza kuipokea.

Filamu sita zilikuwa zikishindanishwa katika kipengele hicho ambapo mbali na Blank Panther ilikuwemo All the Stars, I'll Fight, RBG , The Place Where Lost Things Go, Mary Poppins Returns, Shallow, A Star Is Born, When a Cowboy Trades His Spurs for Wings na The Ballad of Buster Scruggs. 

Filamu hiyo ya Black Panther, mbali ya kutoa mshindi katika kipengele cha muziki wa asili pia imetoa mbunifu bora wa mavazi, tuzo iliyokwenda kwa Ruth Carter na mtayarishaji bora wa filamu aliyoipata Hannah Beachler.

Filamu nyingine iliyong’aa kwa kunyakua tuzo zaidi ya moja ni ile ya Roma, ambayo nayo imetoa mwongozaji bora, picha bora jongefu na matumizi ya lugha ya kigeni ambazo zote zilienda kwa Alfonso Cuaron.

Wakati kwa upande wa waigizaji, Rami Malek, aliibuka mshindi kwa upande wa wanaume kupitia filamu ya ‘Bohemian Rhapsody’, huku Olivia Colman akishinda kwa upande wa wanawake kupitia filamu ya ‘The Favourite’.