Kilichotokea baada ya Mama Diamond kuibiwa simu Viwanja vya posta

MAMA mzazi wa staa wa kimataifa wa muziki wa kizazi kipya nchini, Diamond Platnumz, Bi Sandra maarufu kama Mama Diamond aliibiwa simu katika Viwanja vya Posta jijini Dar es Salaam jana, lakini aliyehusika na tukio hilo alikiona cha moto baada ya kushushiwa kipondo hevi.

Tukio hilo lilitokea jioni wakati wasanii wakiwa wanafanya uhakiki wa sauti katika vyombo vya muziki kwenye Jukwaa La Wasafi Festival kwa ajili ya tamasha.

Mama Diamond alifika katika viwanja hivyo akiwa ameongozana na mumewe Shamte na aliyekuwa Mkurugenzi wa African Stars ‘Twanga Pepeta ‘ Asha Baraka, lakini akiwa anashuka kwenye gari watu walimzunguka ndipo akatokea kijana mmoja alimvamia na kumpora simu kisha kukimbia.

Kijana huyo hakupiga hatua hata kumi kabla ya kuvamiwa na kundi la watu na kuanza kumpiga baada ya kumnyang’anga simu na kama si polisi waliomuokoa habari ingekuwa nyingine. Hata hivyo Mama Diamond aliwaomba polisi wamsamehe kijana hiyo kwa kuwa simu yake ilirudi ila askari hao waligoma.