Asilimia 20 ya mapato tamasha la Wasafi kwenda JKCI. Diamond,Chid Benzi wafunika

Muktasari:

Tamasha la wasafi lahitimishwa, aslimia 20 ya mapato yake kupelekwa JKCI, Diamond,Chid Benzi wafunika

Dar es Salaam. Jana Novemba 9, ndio siku ambayo kilele cha tamasha la Wasafi Festival

2019, lilihitimishwa pale viwanja vya Sayansi  Posta Kijitonyama ambapo wasanii zaidi ya 20 kutoka ndani na nje ya  Tanzania walitumbuiza.

Wakati kwa upande wa viongozi wa Serikali, Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda aliwakilisha huku akitaja moja ya mambo yaliyomkuna kuwa ni pamoja na maamuzi ya waandaaji wa tamasha hilo kuamua asilimia 20 ya mapato yaliyopatikana kupelekwa kuhudumia watoto wanaosumbuliwa na maradhi ya moyo.

Wasafi wanafanya hivi ikiwa in siku chache tangu wachangishe Sh80 milioni kutoka kwa wasanii na wadau mbalimbali kwa ajili ya watoto wanaotakiwa kufanyiwa operesheni katika Taasisi ya moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) na kati ya hizo Diamond Platnumz peke yake alichangia Sh20 milioni

Hata hivyo katika tamasha hilo lililoanza saa 1:00 na kumalizika saa 9:30  usiku, Mwananchi iliyoweka kambi hapo na kubaini  baadhi ya mambo ikiwemo  wasanii  walifunika katika kilele hiko kutokana na shoo zao ambazo walifanya mamia ya watu waliokuwa katika viwanja hivyo kupiga shangwe kila wakati.

 

Diamond habari nyingine

Wasanii wengi walifanya shoo zao mapema kuanzia saa 1:00, usiku lakini habari ilikuwa nyingine baada ya kufika saa 7:13, usiku ambapo msanii Nasib Abdul maarufu kama (Diamond Platinumz), alipopanda katika jukwaa.

Mashabiki wengi walikuwa kama wamepigwa na butwaa baada ya kuona  jukwaani wamepanda wacheza shoo wakiwa wamevalia nguo nyeupe na ghafla muda mfupi alipanda Diamond Platinumz, akianza na nyimbo yake mpya ya Baba lao, hapo ndipo mashabiki walilipuka kwa shangwe la aina yake.

Kuna mashabiki ambao waliamua kuimba sawa na Diamond Platinumz, kuna ambao waliamua kucheza mpaka vumbi kutimuka, kuna ambao waliamua kubebana na wengine kushindwa kujizuia mpaka kupanda jukwaani licha ya  walinzi kuwazuia.

Diamond Platinumz ambaye alikuwa akiachia ngoma baada ya ngoma ndani ya masaa mawili aliyokuwa jukwaani alizidi kuwapagawisha mashabiki baada ya kumpandisha Rayvan na kuanza kuimba nyimbo moja ambayo mashabiki walizidi kufurahi.

Diamond Platinumz ndio kama ameibesha shoo hiyo kutokana kila shabiki alifurahi na vitu ambavyo alikuwa akifanya jukwaani.

 Nyimbo ambazo zilikuwa gumzo ni pamoja na Baba Lao, Kanyaga, na ule ambao Hope alioimba sambamba na  Innoss B mwanamuziki kutoka  Congo

 

Wizkid

Msanii mwingine ambaye alitumbuiza shoo kali alikuwa Mnaigeria Wizkid, ambaye mara baada ya Diamond kumaliza kufanya shoo yake alimkaribisha hapo ndipo mashabiki waliendeleza mzuka ambao walikuwa nao kutoka kwa Diamond.

Wizkid alikuwa akiimba ngoma zake sawa na mashabiki ambao walikuwa wanashangilia na kumfatilia hata pale ikitokea (DJ), amekatisha nyimbo watu waliendelea kuruka na kupiga shangwe mwanzo mwisho.

Shoo ya Wizkid ilizidi kuwa tamu zaidi na kuwakosha mashabiki alipopanda tena Diamond na kuanza kuimba na kucheza wote kwa pamoja zaidi ya dakika 20.

 

Mzee wa bwax

Msanii wa muziki wa Singeli Mzee wa Bwax ni miongoni mwa waliofanya shoo kali na hata mashabiki nao kushindwa kujizuia na kuimba nae hata pale muda ambao kulikuwa mziki umezimwa.

Bwax ambaye alipanda jukwaani saa 2, usiku aliwapagawisha mashabiki wengi ambao walikuwa wakiimba na kucheza nyimbo zake za Kisimu changu laini mbili, Vikao na Upepo wa kisulisuli yaani mpaka vumbi kutimuka katika viwanja hivyo vya Sayansi.

Wakati Bwax anatumbuiza kuna mashabiki ambao waliamua kuvua nguo zao za juu na kuanza kuzungusha kwa mikono, kuna ambao walikuwa wakicheza mpaka kumiminika jasho na wengine kuimba mwanzo mwisho mpaka msanii huyo anashuka jukwaani.

 

Dudu Baya sauti yakauka

Katika hali ya kushangaza msanii Dudu Baya, ilipofika zamu yake jukwaani kwenda kufanya Shoo alijikuta sauti yake imekauka licha ya kuamua kumtambulisha kijina wake mwingine ambaye alidai kawa ni mwanae.

Dudu Baya hakuchukua hata dakika 20, katika shoo yake kwani sauti yake ilionekana kukauka na kuimba pengine kama mashabiki wengi ambao walikuwa katika tamasha hilo walitegemea kutoka kwake.

 

Ferouz, PRO, Jay watingisha

Wasanii wakongwe wa muziki wa kizazi kipa Ferouz ambaye alianza kupanda jukwaani na kibao cha Starehe, alionekana kukonga nyoyo za mashabiki ambao walikuwa wakimba nae sawa na kucheza.

Shoo hiyo na Ferous alionekana kuwa nzuri zaidi baada ya pale alipopanda Prof Jay, na wote kuanza kuimba kwa pamoja nyimbo ambazo waliimba kwa pamoja takribani nusu saa.

TMK ya zamani yashindwa kumimba pamoja, Tiptop wafunika.

Licha ya msanii Diamond kueleza kuwa wanaume TMK ya zamani wangepanda jukwani pamoja, jambo hilo limeshindikana na kila mtu kupanda kivyake

Wakati Temba,KR na wasanii wengine walinaunda TMK wanaume ya sasa walipanda kwa pamoja, Juma Nature yeye alipanda mwenyewe.

Japokuwa kwa upande wa Tiptop walipanda wote, ila alianza kwanza Madee, baadae akawaita Pingu na Denso ambao nao wakikuwa na mzuka ambao uliamsha mashabiki pia.

 

Chid Benz

Pamoja na matatizo aliyowahinkupitia ya kuumwa, Chid Benzi bado amezidi kudhihirisha pumzi yake katika kuimbankila anapoitwa kwenye matamasha.

Kwani katika tamasha hilo la wasafi, Nyimbo yake ya  'Dar es Salaam Stand up' aliyoiachia mwaka 2014, ndio ngoma ya kwanza ambayo iliwavuruga mashabiki wengi waliokuwa katika viwanja hivyo vya Sayansi kwani walikuwa wakicheza na kuimba mwanzo mwisho.

Kwani hata pale alipomaliza kuimba watu walitaka arudie huku wakati huo wakiwa wanarukaruka, wengine walivua mashati, kuna ambao waliinua vitambaa juu kuonyeshwa hisia za namna msanii huyo alivyowakuna.

Pia alisababisha walinzi kupata kazi ya ziada ya  kuwarudisha nyuma mashabiki hao kwa kuwa kadri mzuka ulivyowapanda ndivyo walivyozidi kulisogelea.

Dudu Baya sauti yakauka

Pamoja na wasanii wengine kufanya vizuri, kwa Dudu Baya siku hiyo ilikuwa mbaya kwake kwani  ilipofika zamu yake jukwaani kwenda kufanya Shoo alijikuta sauti yake imekauka.

Pamoja na kusaidiwa na msanii aliyeeleza kuwa ni mtoto wake bado hakuweza kumaliza dakika 20 jukwaani na kukonga nyoyo za mashabiki  kama ambavyo walitegemea kutoka kwake.

Ulinzi wa kutosha

Katika hatua nyingine, mbali ya kuwepo na shoo za maana kutoka kwa wasanii lakini ulinzi ulikuwa wa kutosha katika maeneo yote ambayo shughuli hiyo ilikuwa ikifanyika.

Kulikuwa na maaskari Polisi, Suma JKT ambao ndio walikuwa kama wamemwagwa na mabodigadi ambao nao walikuwa wamevalia suti zao nyeusi wakizunguka katika kila kona kuangalia hali ya usalama.