Babu Tale afichua kwa nini Wasafi inafanikiwa

Monday October 21 2019

 

By Herieth Makwetta, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Mmoja wa mameneja wa WCB, Hamis Shaban maarufu Babu Tale amesema kampuni ya wasafi imejenga misingi imara ndiyo maana inaendelea kujisimamia bila kutetereka na kuendelea kuibua vipaji vya wasanii.

Babu Tale ameyasema hayo leo Jumatatu, Oktoba 21, 2019 wakati wa uzinduzi wa kipindi cha michezo cha Sports Arena kinachowakutanisha watangazaji mashuhuri watano wa michezo akiwemo Edo Kumwembe, Maulid Kitenge, Aboubakar Mkude, Mwanaidi Suleiman na Ahmed Abdalah.

Amesema akiwa meneja wa kwanza alihakikisha kampuni hiyo inajenga uimara katika shughuli zake na tangu kuanza upande wa muziki wamefanikiwa kuanzisha kampuni na kusimamia wasanii, kurekodi video na shughuli zingine.

“Tuna mipango iliyo thabiti katika kuhakikisha jambo lolote tunalolifanya linafuata taratibu, kujipanga ndiyo siri ya mafanikio siku zote,” amesema.

Babu Tale amesema licha ya shughuli za muziki kampuni hiyo inazidi kukua na sasa inaingia kimataifa baada ya kufungua redio na Televisheni ambayo inatarajia kuanza kuonekana duniani kupitia DSTV.

“Siku zote mafanikio hayajawahi kutufanya tukabweteka wala kuvimba vichwa, jana Diamond kapata tuzo, Rayvann amepata pia tuzo ya mwanamuziki bora Afrika lakini hii inatufanya tusonge mbele zaidi, haturidhiki na mafanikio tunayoyapata,” amesema Babu Tale.

Advertisement

Tukio hilo limehudhuriwa na watu wengi mashuhuri katika mpira wa miguu nchini na mgeni rasmi ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, DkHarrison Mwakyembe.

Advertisement