Babu Tale ampongeza Fid Q kwa kufunga ndoa

Wednesday January 2 2019

 

By Nasra Abdallah, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Meneja wa lebo ya Wasafi, Babu Tale amempongeza msanii Fareed Kubanda ‘Fid Q’ kwa kufunga ndoa na mpenzi wake wa siku nyingi, Karima.

Ndoa hiyo ilifungwa jana Januari Mosi 2019 katika  msikiti wa Qiblatain uliopo Boko jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na wasanii mbalimbali akiwemo Ambwene Yesaya 'AY'.

Baadhi ya watu waliompongeza mkali huyo wa Hip Hop ni Babu Tale ambaye siku za hivi karibuni aliingia katika malumbano na Fid Q.

Mvutano baina yao uliibuka baada ya Tale kushangazwa na Fid Q kulifagilia Tamasha la Fiesta, akieleza kuwa pamoja na ukongw, Fid Q hana hata gari na anaishi kwa kumtegemea mwanamke.

Katika majibu yake Fid Q alisema maendeleo si kuwa na gari na kuahidi kuyaonyesha hadharani magari aliyonayo.

Kuhusu kumtegemea mwanamke alisema pengine ni chakula kitamu ambacho Tale alipikiwa na mkewe siku alipowatembelea, huenda Tale alidhani hata aliyekinunua chakula hicho alikuwa mwanamke huyo.

Katika ukurasa wake wa leo wa Instagram, Babu Tale aliweka picha y Fid Q na kuandika, “Hongera mtani Fid Q na karibu kundini, Mungu awasimamie kuilinda ndoa yenu maana kwenye imani ya dini yetu hapa umepanda daraja.”

"Kama nakuona utakavyopasuka maana mama kwa kutoa kitu hatari nakumbuka ule msosi hadi watu wakafungwa karata kwa utamu wa chakula.”

Advertisement