VIDEO: Basata washangaa wanaohoji mapokezi ya Diamond nje ya nchi

Basata washangaa wanaohoji mapokezi ya Diamond nje ya nchi

Muktasari:

Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) limeponda tabia za baadhi ya watu wanaobeza mapokezi ya msanii wa Tanzania, Diamond Platnumz katika ziara za muziki nchi za Afrika Magharibi.

Dar es Salaam. Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) limeponda tabia za baadhi ya watu wanaobeza mapokezi ya msanii wa Tanzania, Diamond Platnumz katika ziara za muziki nchi za Afrika Magharibi.

Hivi karibuni akiwa nchini Sierra Leone, Diamond aliweka video kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram na kuonyesha namna wananchi wa huko walivyompokea.

Mmoja wa mameneja wake, Babu Tale aliweka video ya Diamond akiwa jukwaani katika tamasha la Jamafest na kutaka asifananishwe na wanamuziki wengine.

Maelezo ya wawili hao yaliwaibua mashabiki waliowashambulia na baadhi kusema onyesho la Jamafest lilihusisha wasanii wengi si Diamond pekee, kwamba msanii huyo kudai ameujaza uwanja si sahihi.

Katibu Mtendaji wa baraza hilo, Geofrey Mngereza amesema kitendo hicho kimewasikitisha na kuwataka Watanzania kubadilika.

Amesema alitarajia kuona watu wakimpongeza Diamond kwa hatua aliyopiga kwenye muziki, “nchi anazokwenda hawazungumzi Kiswahili lakini kupitia muziki wake watu watakijua Kiswahili.”

“Tupende tusipende Diamond anaipeperusha bendera ya Tanzania na anapendwa. Ninawapongeza  waliompokea katika nchi hizo.”

Amesema kuna wakati wasanii wanalaumiwa bila sababu wanapokwenda nje ya mipaka kushiriki mashindano mbalimbali  na kuona jukumu la ushindi ni la kwao peke yao.

“Hata kunapokuwa na mashindano ambayo wananchi wanatakiwa kupiga kura kunakuwa na uzito wa kufanya hivyo, wengi wakiamini ni ushindi wa washiriki na hauwahusu, nchi jirani zinatushinda mara nyingi kwa sababu hiyo,” amesema.

“Tuungane kwa pamoja tupende kilicho chetu kwani Diamond hawezi kuwa Mkenya au Mganda ni Mtanzania mwenzetu,  anapofanya jambo zuri anatuletea sifa nchi yetu hakuna budi kumpongeza na kumpa moyo.”