Beresa Kakere akutwa amefariki chumbani

MWIMBAJI mkongwe wa muziki wa dansi nchini, Beresa Kakere Leo Jumatano asubuhi amekutwa amefariki chumbani kwake ilhali akiwa hana jeraha lolote.
Mdogo wa mwanamuziki huyo ambaye naye ni mwanamuziki wa dansi, Juma Kakere, amethibitisha kutokea kwa kifo cha kaka yake.
Juma Kakere alisema kaka yake amefariki dunia asubuhi Tanga Barabara ya Nne katika chumba alichokuwa akiishi baada ya majirani zake kugundua maiti yake walipovunja mlango.
“Alikuwa amechelewa kuamka, wakamgongea mlango bila ya mfanikio ndipo wakavunja na kumkuta amefariki dunia,” alisema Juma Kakere akiwa safarini kwenda Tanga.
Juma alisema mara ya mwisho kuwa na kaka yake ilikuwa wiki mbili zilizopita na hakuwa akiiumwa, bali amefariki ghafla.
“Kwa kweli kaka yangu Beresa ni mtu ambaye alinisapoti katika kazi yangu ya muziki na ndiye aliyegundua kipaji change na alikuwa anajitahidi sana kuimba nyimbo zangu nilizokuwa nikizitunga kabla sijawa mwanamuziki,” alisema Juma.
Kakere alizaliwa Tanga na alimaliza masomo yake katika Shule ya Sekondari ya Karimjee mwaka 1969.
Marehemu alianza kujifunza muziki katika Bendi ya Jamhuri Jazz chini ya John Kijiko na baadaye  alipiga muziki katika bendi mbalimbali za Nairobi na Mombasa za Kenya.
Alirejea nchini mwaka 1976 alipojiunga na Biashara Jazz na kutamba na Kibao cha Clara.
Januari, 1978 aliingia studio na Bendi ya Dar International na kurekodi nyimbo kadhaa ukiwamo utunzi wake wa Magreti.
Mwaka 1979, alijiunga na  Juwata Jazz akiwa na marehemu Kassimu Mponda na kupata umaarufu mkubwa alipotunga kibao cha Sogea Karibu na vingine vya Utu ni Tabia Njema na  Nimekubali Makosa.
Hata hivyo, hakudumu sana katika bendi hiyo baadaye alijiunga na Bima Lee na kutamba na nyimbo za Asia, Remmy, Ombi na nyingine nyingi hadi alipoamua kustaafu shughuli za muziki mwaka 1982.
Kwa mujibu Juma Kakere, Beresa hakuacha mke wala mtoto.