Ndani ya Boksi: Darassa mpaka ale unga ili tumuelewe?

Saturday March 28 2020
darasa pic

Kwa miaka mingi sana sijawahi kuona mrembo aina ya Khadija. Nilipigwa upofu nikashikwa ganzi. Nikakolea mpaka nikaisahau hata nafsi yangu. Muombe Mungu wako yasikukute yaliyonikuta. Si kwa ubaya, bali kwa hisia kali juu yake. Inavutia zaidi kusimuliwa kuliko kusimulia. Acha watu wengine wajinyonge kwa sababu ya huba.

Sikuwa mgeni wa penzi, bali nakiri nilikuwa mgeni wa urembo wa aina ile. Tangu miaka ya 1995 hadi 2020 Khadija anabaki kuwa mrembo bora katika utawala wa ubongo wangu. Na kuna vivutio vingi vimeongezeka kwake.

Kuna vitu vinasimulika kirahisi. Unataka nikusimulie maisha ya ustaa wa Kanumba? Wakati huo akitawala magazetini, runingani, blogs mpaka mitandaoni? Ni kazi rahisi sana kama kuchana ‘tishu’ iliyoloa. Lakini urembo wa Khadija ni jukumu zito. Kama vipi nyie mtoeni tu huko jela. Mimi siwezi kusimulia. Ni mrembo sana.

Wakati mwingine Dar es Salaam inakosa mvuto. Kwa sababu ya ukosefu wa viumbe sampuli hii. Kina Delilah wa kunogesha mitaa kila kona ya jiji wako Segerea mwaka wa nane sasa. ‘Ene wei’ hii haina maana kuwa huku mtaani hawapo. Wapo tena wengi wakizaliwa kila uchwao.

Tatizo nililonalo ni lilelile tulilonalo Wabongo. Tuna hulka ya kukariri kitu. Tukishakariri jambo hatutaki kujua upande wa pili ukoje, hatutaki kubadilika, hata tukibadilika basi inakuwa jumla, tunasahau yale ya nyuma. Tabia hii inatufanya tuwe kama baiskeli ya ‘jimu’. Unanyonga pedeli kwa kasi ukiwa palepale. Ndo Wabongo tulivyo.

Nyakati za nyuma tulisombwa na mafuriko ya Wakongo mpaka tukawapuuza wazee wetu wale wa Msondo na wenzao. Tukawa mateka wa Wakongo na Kibinda Nkoi, Kwasa Kwasa, Nzawise, Ndombolo na Chamukware. Huku majina kama Dalikimoko yakiwa kama sala nyakati za kulala kuamka na kupata msosi.

Advertisement

Nani hakumjua Pepe Kalle, Madilu, Yondo Sister mpaka Bileku Mpasi? Hatukuwa mashabiki tu. Tulikuwa wafuasi, wafurukutwa, wakereketwa na mateka wao. Si waimbaji tu, hadi wapiga tumba na kinanda tukawajua. Wakawa mastaa midomoni mwetu. Katika utawala wa bolingo nani akumbuke uwepo wa Bima Lee na MK Group?

Kama ilivyo kwangu kujisahau na kuamini hakuna mwanamke kama Khadija. Ndivyo ilivyokuwa kwa Wabongo kuamini Bolingo ndo muziki bora zaidi. Kuna wakati ‘Wasauzi’ walituteka na kuwaweka kando kina JB Mpiana na Awilo Longomba. Tukawa machizi Kwaito ile ile ya kina Brenda Fassie. Kabla ya ujio wa Bongofleva.

Ukaja muziki wa kizazi kipya na kuua upuuzi wote wa bolingo, kwaito, zuku mpaka Reggae. Kila kitu kikawa ni Bongofleva. Kuanzia mitaa ya Kinondoni, Kibera mpaka Entebe. Kila kijana alitamani kuwa staa wa Bongofleva. Mpaka fundi uwashi, seremala, mwalimu wa sayansikimu wengi wao walitamani maisha ya Ubongofleva.

Lakini sasa mambo yamebadilika kuanzia mashabiki na wanamuziki wetu wenyewe wote tumekuwa mashabiki wa kusikiliza midundo ya Kinaijeria. Na wanamuziki wetu nao wanahusudu kuimbia midundo ya Kinaijeria. Runinga, redio na ‘madijei’ kwenye vibaa vya Uswahilini wote wametekwa na Unaijeria. Hili ni tatizo sana.

Wakati unataka kumlaumu ‘dijei’ kwa kupiga ngoma za Kinaijeria tu kuna mwingine anamuulizia ‘dijei’ kwa nini haweki ngoma za Nigeria? Tulilazimishwa kuzipenda na sasa tunawalazimisha kuzipenda. Ndo maana wasanii wetu wamekuwa na Unaijeria mwingi kwenye nyimbo zao. Wafanyaje na ndo kitu wengi wetu tunataka?

Ndo maana kuna wasanii wengi wanafanya vizuri, tena bila uwepo wa Unaijeria kwenye midundo na sauti. Lakini hawapati fursa ya kuonwa na kuongelewa sana. Kwa sababu masikio na macho yetu yameelekezwa sehemu moja. Kama mimi na Khadija wangu hatuoni upande wa pili kile kinachoendelea, tumeshikwa, tumetekwa haswa.

Darassa ni miongoni mwa watu ambao wamesimama katika asili ile ya Ubongofleva na yeye ana aina ya mitambao yake ambayo ni yeye pekee anayefanya hivyo. Lakini pamoja na kufanya ngoma kali kuanzia mwaka jana ni kama watu hawaoni. Lile jamaa linapambana aiseee! Lakini hapati ‘bigi taimu sapoti’ kwa ubora ule ule wa ngoma zake. Tumekariri Unaijeria.

Juzi kati nimeona ngoma mpya ya Darassa aliyoshirikishwa na mchizi wa Kikenya Nameless. Bonge moja la ngoma. Midundo na mitambao ile ile ya Bongofleva. Humo ndani Darassa kapita kikatili utadhani ngoma ni mali yake pekee. Ukiwa mtu wa muziki utaona utofauti.

Lakini Wabongo kwa sasa fleva zetu tamu masikioni ni zile za kutoka Abuja na Lagos. Wametuteka mno hatuoni anachofanya Darassa kwa sasa. Fuatilia ngoma zake kuanzia mwaka jana hadi hivi sasa. Utashangaa kwa nini mtaani hana uzito ule? Bahati mbaya sana Darassa kakutana na kizazi mkurabita, kile kinachotaka vitu tofauti na kile anachofanya. Inaumiza kuona tetesi za Darassa kutumia unga zilivuma na kusambaa haraka kuliko taarifa za ubora wa ngoma yake na Jux. Mchizi katoa ngoma dabodabo zenye ujazo na ubora wa hali ya juu lakini mapokeo si yale.

Mapokeo ni mazuri lakini si kivile kwa ukubwa wa ngoma husika. Matokeo yake Nameless anachizika na kipaji na voko la mchizi kuliko Lusajo wa Magomeni Usalama. Kwa nini? Tunasubiri fleva za Unaijeria na kiki za kidwanzi kule Kenya wamemuelewa mpaka wanaamua kumpa shavu mchizi, sisi huku tumekariri.

Tuna vipaji vya kusambaza taarifa mbaya kuliko njema. Ndo maana tulionyesha ushirikiano kwa tetesi za kubwia unga kuliko ubora wa muziki wake. Midomo na masikio yetu yana upendo wa agape na simulizi mbaya za watu. Stori za unga ni baada ya ukimya wa muda mrefu wa Darassa kisanii tukaamua kumzushia mwana.

Tungekuwa tunashirikiana vilevile kusambaza taarifa njema leo Darassa angekuwa anakunja noti nyingi kupitia views za YouTube. Lakini mema ya mtu hayana nafasi kwenye bongo zetu. Tunataka kusikia msela kakata ringi. Hana chapaa, kakosa dira na hana hata ujanja wa kuchukua bodaboda kitaa. Hizo ndo stori zetu pendwa.

Tunahusudu michapo ya kichawi zaidi. Kumtakia mabaya mtu ni sehemu ya ushirikina ambao tunatakiwa kuwaachia wale wanaoabudu shetani na kazi zake. Kama tunapenda sana stori mbaya juu ya watu pia kwa kiwango kile kile tupende stori zao njema lakini kilichopo Wabongo hatuko ‘fea’, tunakariri sana kwamba maisha ya muziki bila skendo ni ngumu. Yaani uzushe jambo ili ‘utrendi’ ndipo uachie ngoma ikimbize. Tunafanya maisha yawe magumu bila sababu. Tumekariri kiki. Tumetekwa nazo, tumelishwa limbwata na kufanywa mazuzu wa kiki. Tumekariri kwamba fulani kamuacha demu wake? Basi ana ngoma mpya. Siyo poa aiseee!!.

Advertisement