Diamond, Harmonize kukutana kwenye tuzo Soundcity MVP?

Muktasari:

Tuzo za Soundcity MVP zinatarajiwa kufanyika usiku leo nchini Nigeria, huku swali likiwa ni je Diamond na Harmonize watakutana kwa mara ya kwanza tangu Konde Boy ajitoe katika lebo ya WCB? Jibu kama ndiyo au hapana muda utaamua.

Dar es Salaam. Macho na masikio leo Jumamosi Januari 11, 2020 yapo katika tuzo za Soundcity MVP zitakazofanyika ukumbi wa Eko Convention Centre jijini Lagos nchini  Nigeria.

Tuzo hizo ambazo ni za kwanza kufungua mwaka 2020 nchini Nigeria, zitawashindanisha wasanii mbalimbali kutoka Afrika ambapo vipengele 15 vitawaniwa.

Mbali ya yote tukio linalosubiriwa kwa hamu na mashabiki wa burudani ni iwapo wasanii Diamond Platnumz na Harmonize watakutana katika hafla hiyo ya utoaji tuzo usiku wa leo.

Tayari Diamond ameshathibitisha kuwapo ambapo mbali ya kuwania tuzo  pia atatumbuiza pamoja na Davido, Wizkid huku Harmonize mpaka sasa akiwa hajathibitisha ushiriki wake na alipotafutwa kwa ajili ya kuzungumzia hilo hakupokea simu.

Iwapo mmoja kati yao hatatokea katika hafla hiyo itakuwa ni mara ya  pili wawili hao wanatajwa katika tuzo, lakini hawatokei au hawakutani ikiwamo ile ya African Muzik Magazine Award (AFRIMMA), iliyofanyika Oktoba 2019 nchini Marekani.

Ingawa Diamond alisema hakuhudhuria hafla hizo kwa sababu mameneja wake hawakumalizana kiasi cha kukubaliana na watayarishaji wa tuzo hizo.

Tangu Harmonize atangaze kujiondoa katika lebo ya Wasafi (WCB), Agosti 2019 hawajawahi kukutana pamoja na Diamond ambaye ni Mkurugenzi wa WCB.

Katika hafla ya utoaji wa tuzo hizo Diamond anawania vitatu  ikiwemo msanii bora wa Afrika, msanii wa kidigital na msanii bora wa kiume.

Pia staa huyo wa kibao ‘Baba lao’ ametajwa kuwania kipengele cha chaguo la msikilizaji, kupitia wimbo wa ‘Kainama’ alioimba kwa kushirikiana na msanii Harmonize na Burna Boy.

Wimbo ‘Kainama’, uliachiwa Machi, 2019 ambapo ulifanya vizuri.

Wasanii wengine wa Tanzania waliotajwa katika tuzo hizo ni Rayvanny na Nandy katika kipengele cha msanii bora wa Pop na mtengenezaji wa muziki S2Kizzy katika kipengele cha mtengenezaji bora wa muziki.

Kama vile haitoshi wimbo wa ‘Tetema’ alioimba Rayvanny kwa kumshirikisha Diamond umetajwa katika vipengele viwili ikiwemo wimbo wa mwaka na chaguo la watazamaji.

Mwananchi inawatakia kila la kheri wasanii hao kurudi na ushindi.