Diamond akwepa kumzungumzia Tanasha

Muktasari:

Leo Jumatano Machi 4, 2020 katika mkutano na waandishi wa habari ambao Diamond ametangazwa kuwa balozi wa rangi za Coral Paints, msanii huyo amekwepa kuzungumzia kuhusu suala hilo.

Dar es Salaam. Kama ni mfuatiliaji wa mitandao ya kijamii ni wazi kuwa hujapitwa na uvumi wa msanii Diamond kuachana na mpenzi wake Tanasha Donna.

Tetesi za kuachana kwa wawili hao wanaotesa na wimbo wa Gere kwa sasa zilianza juzi Jumatatu Februari 2, 2020 katika mitandao ya kijamii baada ya Tanasha kwa nyakati tofauti kuweka ujumbe mbalimbali uliotafsiriwa kuwa ni vijembe kwa Diamond.

Leo Jumatano Machi 4, 2020 katika mkutano na waandishi wa habari ambao Diamond ametangazwa kuwa balozi wa rangi za Coral Paints, msanii huyo amekwepa kuzungumzia kuhusu suala hilo.

Jana katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram, Diamond aliandika, “kila mtu ana story yake unataka kujua ya kwangu,” jambo ambalo liliibua maswali, waandishi wa habari kutumia mkutano huo kumuuliza kuhusu uhusiano wake na Tanasha.

Licha ya kuulizwa swali hilo, Diamond alikwepa na badala yake kujikita kujibu yanayohusu rangi.

Hata baada ya kumalizika kwa mkutano huo waandishi walimfuata pembeni na kumuuliza kuhusu suala hilo lakini aliwajibu kwa kifupi, “achaneni na habari hizo.”

Katika mkutano huo Diamond aliambatana na mameja wake watatu, Babu Tale, Sallam SK na Mkubwa Fella.

Mahusiano njia panda

Mbali na vijembe, Tanasha  amekuwa akifuta baadhi ya picha kwenye ukurasa  wake zinazomuhusisha Diamond ikiwemo ile ya nyimbo yake mpya ya 'Jeje' aliyoiachia wiki iliyopita.


“Having a clean heart is Priceless because it’s so damn valuable that not even money can match up to its standards” aliandika Tanasha kwenye mtandao wa Instagram ikiwa na maana ya kuwa na moyo safi hakuna bei kwa sababu ni muhimu sana hata pesa haziwezi kulingana na viwango vyake.

Kauli hiyo ilianza  kutafsiriwa kama vijembe kwa mwenza wake huyo.
Watu wa mitandao wamekuwa wakitafsiri hatua hiyo na maneno hayo ambayo amekuwa akiyaandika kama tayari Tanasha kaamua kuachana na Diamond ambaye walijaliwa kupata naye mtoto mmoja.
Kama vile haitoshi Tanasha ambaye mbali ya kuwa mwanamuziki ni video vixen na mtangazaji nchini Kenya, amekata mawasiliano na mama na dada yake Diamond kwenye ukurasa wake wa Instagram ambapo mtu ukiingia humo inasomeka  'unfollow' na 'block'.
Pia jana  aliongeza idadi ya watu alioamua kukata nao mawasilano wengi wakiwa wale walio karibu na Diamond, wakiwemo wasanii wa lebo ya WCB.

Kati ya hao wapo wasanii wa Bongofleva, Mbosso, Queen Darleen na Ray Vanny.
Hata hivyo, Mwananchi ilimtafuta Dada wa Diamond, Esma Platnumz ili kupata ukweli kuhusiana na jambo hilo ambalo kwa siku mbili hizi limekuwa gumzo katika mitandao ya kijamii
Katika majibu yake alijibu kwa kifupi “mimi sijui kwanza nimelala saa hizi,” kisha akakata simu.