Diamond anaandaa albamu ya Rais Magufuli

Muktasari:

Baada ya kibwagizo katika Baba Lao, Diamond kuja na albamu maalum kwa ajili ya Rais wa Tanzania, John Magufuli,  meneja wake ajigamba itakuwa na nyimbo pendwa. Tanzania inafanya uchaguzi mkuu mwaka 2020 ambao utahusisha uchaguzi wa madiwani, wabunge na Rais.

Dar es Salaam. Kama umeusikiliza wimbo wa msanii wa muziki nchini Tanzania, Diamond ‘Baba Lao’ hakuna shaka umekutana na mstari unasema Magufuli baba lao. Ni mstari uliokuwa na maana ya kumsifia Rais John Magufuli.

Habari ni kwamba sifa hizo hazijaishia hapo kutoka kwa Diamond kwani yuko mbioni kuachia albamu itakayosheheni nyimbo za aina hiyo.

Meneja wa Diamond, Hamis Taletale ‘Babu Tale’ amesema tangu Baba Lao utoke umekuwa wimbo pendwa kwa wananchi na unatumika kumkaribisha Rais kwenye maeneo anayotembelea.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram Babutale amedokeza kuhusu ujio huo wa albamu maalum ya Rais Magufuli.

Babutale ameweka video ya msemaji wa CCM akiimba kipande hicho na ujumbe uliosomeka, “Si kila mtu kaumbiwa taaluma ama uwezo wa kushawishi au kuvumisha jambo. Hivyo waambieni kuwa kuna kufanya wimbo wa chama na kuna kufanya wimbo pendwa wa chama, wenye kuvuma na ushawishi kila kona,

Akaendelea, “hii ilikuwa teaser tu ya kumsifu rais wetu Magufuli lakini ndio imekuwa wimbo pendwa kwa wananchi wote na kila rais wetu atembeleapo sehemu watu wamekuwa wakimuimbia au kutamani kumkaribisha na wimbo huu. Niwajuze kuwa kijana wenu Diamond kishamaliza albamu maalum kwa ajili ya rais Magufuli, soon nitawaambia lini itakuwa hewani,”.

Mashabiki wametafsiri maneno hayo ya Babu Tale kama kijembe kwa Harmonize ambaye mwishoni mwa mwaka jana aliachia wimbo uitwao ‘Magufuli’ ikiwa ni remix ya Kwangwaru.

Sanjari na Harmonize wasanii wengine wa muziki wa kizazi kipya walioimba nyimbo za aina hiyo ni Nandy na Beka Flavour.