Diamond atoa ujumbe kwa wasanii wenzake Tanzania- Video

Diamond atoa ujumbe kwa wasanii wenzake Tanzania- Video

Muktasari:

  • Tamasha la Wasafi nchini Tanzania lilihitimishwa Jumamosi iliyopita ya Novemba 9, 2019 ambapo Msanii Diamond amewashukuru wasanii wenzake walioshiriki tamasha hilo huku akiwaomba kuepuka kuchonganishwa.

Dar es Salaam. Msanii wa muziki nchini Tanzania, Diamond Platinumz amewataka wasanii wenzake kutokubali kuchonganishwa na kugombanishwa jambo ambalo halina tija kwa sanaa.

Kauli hiyo ya Diamond imekuja baada ya kuwashukuru wasanii wenzake wa ndani na nje ya Tanzania walioshiriki Wasafi Festival kwa kuleta mapinduzi katika tasania ya burudani nchini humo.

Amesema kwa muda mrefu kumekuwa na dhana ya ugomvi lakini tamasha la Wasafi lililohitimishwa jijini Dar es Salaam Jumamosi iliyopita Novemba 9, 2019 limekwenda kufuta dosari hiyo.

“Zamani kulikuwa na mambo ya uchonganishi, tulikuwa hatuendi kwenye shoo za wenzetu. Kupitia wasafi festival tumeifuta hiyo na nyie mkiwa na shughuli zenu nialikeni, tunavyojiweka mbali ndio tunatengenezewa maneno ya uchonganishi.”

“Tunachonganishwa vitu vya uwongo na kweli tunachukiana wakati kila mtu ana mafanikio yake katika sehemu yake,” amesema Diamond

Kuhusu ushiriki wa wasanii katika tamasha lake, amesema alijaribu kuwafikia wengi wao lengo likiwa kuwapa fursa na kuwapa burudani mashabiki.

“Nawashukuru wasanii kwa kuniunga mkono, tuendelee na ushirikiano huu hata katika kazi zenu. Mashabiki ni wetu sote na walishiriki kutushangilia kwa pamoja hakuna mwenye mashabiki wa mtu mmoja,” amesema Diamond.