Ebitoke kushiriki Miss Tanzania 2020

Muktasari:

Msanii wa filamu za vichekesho nchini Tanzania, Annastazia Exavery (22) maarufu Ebitoke amesema atashiriki shindano la Miss Tanzania mwaka 2020.

Dar es Salaam. Msanii wa filamu za vichekesho nchini Tanzania, Annastazia Exavery (22) maarufu Ebitoke amesema atashiriki shindano la Miss Tanzania mwaka 2020.

Akizungumza leo Ijumaa Februari 28, 2020 Ebitoke ametaja sababu tatu za kushiriki shindano hilo, “sababu ya kwanza mimi ni mrembo nisingependa kutumia urembo huu kwa mambo mengine yasiyokuwa na tija, ndio maana nimeamua kushiriki kwa kuwa kuna fursa nyingi.”

“Pili nataka kuwaonyesha vijana kuwa hakuna kinachoshindikana kama mtu ukiamua, hii itasaidia wengi kujiamini na kushiriki. Tatu, mimi ni msanii napaswa kubadilika. Katika urembo ni moja  ya njia kuonyesha kipaji changu kingine mbali ya kuigiza filamu na vichekesho.”

Mwandaaji  wa shindano hilo, Basila Mwanukuzi amethibitisha ushiriki wa Ebitoke akibainisha kuwa amerudisha fomu jana.

Msanii huyo amejizolea umaarufu kutokana na kuigiza vichekesho akitumia lafudhi ya kabila la Wahaya.

Washiriki wanapatikanaje

Jana katika mkutano wake na waandishi wa habari, Basila amesema kamati ya Miss Tanzania imeachana na utaratibu wa zamani wa mawakala kutafuta washiriki wa shindano hilo na badala yake itazunguka katika kanda zote nchini kuwafanyia usahili.

Amesema utaratibu huo mpya wa kutafuta warembo watakaoshiriki shindano la Miss Tanzania unatarajiwa kuanza Machi, 2020.

Amesema utaratibu huo utasaidia  kuondoa changamoto mbalimbali zilizojitokeza kwa baadhi ya mawakala ambao hawakuwa waaminifu.

Amezitaja changamoto hizo kuwa ni kusimamia warembo, utoaji wa zawadi, kujaza na urudishaji  fomu kwa wakati ili warembo waweze kufanyiwa usahili.

“Usahili utaanza Kanda ya kati Machi 7 jijini Dodoma, Kanda ya Kaskazini Machi 14, Kanda ya Ziwa Machi 28, Kanda ya Mashariki Aprili 4. Kanda ya vyuo vikuu Aprili 21, Kanda ya nyanda za juu Kusini Aprili 11 na Kanda ya Dar es Salaam itakuwa Mei 2, 2020,”amesema mkurugenzi huyo katika mkutano wake na waandishi wa habari.

Amesema Miss Tanzania mwaka 2020 itajikita  kutangaza misitu na utalii wa asili, uhamasishaji wa kupanda miti katika kila kanda.