Fainali tamasha la Fiesta 2019 lilivyoacha gumzo Dar

Tuesday December 10 2019

 

By Kalunde Jamal, Mwananchi [email protected]

Katika hali isiyotarajiwa na wengi, hususani kundi la vijana, ni kuendelea kupenda kazi za wasanii wakongwe na nyimbo za muda mrefu kuliko mpya.

Hilo liliendelea kujidhirisha juzi usiku katika tamasha la Tigo Fiesta ambalo fainali yake ilikuwa Uwanja wa Uhuru, ikiwa ni siku chache baadaye ya tamasha jingine la Wasafi kutawaliwa na nyota wa zamani wa Bongo Fleva.

Msanii nyota wa Hip Hop ambaye pia ni mbunge wa Mikumi, Profesa Jay aliiongoza kundi la wasanii wa miaka ya tisini ambao nyimbo zao zilitia fora usiku huo, akiunganisha nyimbo nne, zikiwemo maarufu za “Piga Makofi” na “Kamili Gado” na wakati mwingine kuachia mashabiki waimbe sehemu kubwa ya nyimbo hizo.

Mwingine ni Ney wa Mitego aliyeamsha mashabiki na nyimbo zake tatu; “Mungu Anakuona” na “Nataka Kuwasha Moto”.

Wakati Profesa Jay na Ney waliwakilisha kundi la wasanii wa rap walioamsha mashabiki, Barnaba Boy aliwafanya walipuke kelele alipoanza kuimba nyimbo mpya walishangilia, lakini walilipuka zaidi alipoimba nyimbo za kitambo.

“Nimeshajua, mnataka niwakumbushe zamani,” alisema alipoanza kuimba nyimbo za enzi zake hizo, akianzia na “Nitakupenda milele Daima”, “Amekosea Namba” huku akizichanganya.

Advertisement

Hali ilikuwa tofauti kwa wasanii waliokuwa wakisubiriwa kwa hamu kama Ali Kiba na Harmonize ambao mashabiki waliimba nao pamoja nyimbo zao mpya na za zamani.

Mashabiki na vituko vyao

Ukiacha mashabiki wachache ambao walikuwa wamechangamka na kinywaji, wengi wao walilala uwanaani kusubiri wanamuziki nyota ambao walianza jkupandaa saa 5:35 usiku kwa kuanzia na Benson na kufuatiwa na Jay Melody.

Kwa wasanii wa kike, ukiacha Nandy, waliofanya vizuri ni pamoja na Ruby, lakini sifa nyingi zilikwenda kwa Maua Sama.

Muda mfupi baada ya Maua kupanda jukwaani, mvua ilianza kunyesha, lakini hakuzubaa wala kuyumba.

Aliimba nyimbo kama “Niteke”, “Gusanisha” akiwa na G Nako kiasi cha kuwabakisha mashabiki uwanjani wakicheza huku wakinyeshewa.

Maua aliuteka uwanja hata wale waliokimbia mvua na kujikinga nje ya uwanja, bado walikuwa wanaimba na kucheza pamoja naye.

Naye Young D alikumbana na tukio la mashabiki kumvuta kutoka jukwaani mara tu baada ya kuwasalimia hadi askari walipofanikiwa kumrudisha jukwaani.

Katika purukushani hiyo raba moja aliyovaa ilivuliwa, jambo lililomlazimu kuvua na nyingine na kuwarushia.

Mashabiki ni kama walikuwa wanamsubiri Ali Kiba na Harmonize waimbe ndipo waondoke, kwa kuwa saa 9:30 usiku walikuwa wametulia, baada ya Ali Kiba kuanza kutumbuiza na baadaye Harmonize.

Ali Kiba aadhimisha miaka 17

Kiba, ambaye kwa sasa anatamba na kibao cha “Mshumaa”, alitumia tamasha hilo kuadhimisha miaka 17 tangu aingie katika muziki wa kizazi kipya na mashabiki walimpa zawadi maalumu.

“Wimbo huu ni zawadi kwa jasiri mwongoza njia Ruge Mutahaba aliyetangulia mbele ya haki ambaye hakuwa tayari kuona vijana wanabaki na vipaji vyao, kwa kuwa aliwasaidia wengi,” alisema Kiba akizungumzia wimbo wa “Mshumaa”.

Kwa mara nyingine, wasanii takriba wote waliendelea kutumbuiza kwa kutumia muziki uliorekodiwa, hali ambayo huwafanya wakati mwingine wasiende sawia na mambo ambayo wanataka kushiriikisha mashabiki.

Wengi walitumia nyimbo ambazo zimerekodiwa kwa ajili ya kuchezwa katika redio na TV na hivyo sauti zao jukwaani kutoenda sambamba na waitikiaji wa nyimbo hizo, tofauti na kama wangetumia ala za muziki katika matamasha.

Hali ilikuwa kama hiyo katika tamasha la Wasafi ambao walifanyia tamasha lao Chuo cha Posta, Mikocheni jijini Dar es Salaam.

Shilole haachani na jiko

Staa anayetamba katika kiwanda cha filamu na muziki, Shilole ni kama haachani na jiko baada ya kupanda jukwaani na sahani na bakuli ya chakula na kupakua huku akiwagawia baadhi ya mashabiki jukwaani hapo.

Pamoja na kuimba nyimbo nyingi, ulioamsha shangwe wengi ni ule aliyoshirikishwa na Baddest 47 wa “Nikagongee” ambao unapendwa na vijana wengi kwa sasa.

Kuwapo kwa tamasha hilo kwenye eneo la Uwanja Uhuru Temeke, jijini Dar es Salaam kulisisimua kwa muda uchumi katika eneo hilo.

Nje ya uwanja, mwenye maji, karanga, samaki na hata mama lishe, walinufaika kwa muda wa saa nane hadi kumi.

Mbali na hao wengine walionufaika ni wenye biashara ndogondogo, waendesha vifaa vya moto ikiwamo bajaji, pikipiki, daladala ambazo zilikesha hadi saa 12:00 asubuhi zikibeba abiria waliokuwa wakitoka na kuingia uwanjani hapo.

Ulinzi

Kama kuna jambo la maana limefanyika katika tamasha la Tigo Fiesta 2019 ni kuwapo na ulinzi wa kutosha ndani na nje ya uwanja ambapo gari ya washawasha ilikuwa ikizunguka nje na ndani ya uwanja, huku kukiwa na Polisi wa kutosha.

Baada ya mashabiki wengi kuanza kuondoka Polisi walijipanga katika eneo na nje ya uwanja na kupiga filimbi kwenye maeneo yaliyo na giza kuwatimua vijana waliojipanga kufanya uhalifu.

Mwananchi ilishuhudia vijana zaidi ya watano, wakiwa wamekamatwa kwa nyakati tofauti kutokana na kukwapua simu za mashabiki waliojitokeza uwanjani hapo.

Kama hiyo haitoshi kulikuwa na gari ya wagonjwa ambayo ilifanya kazi ya ziada kubeba watu waliozimia wakiwamo waliolewa kupitiliza.

Pia Mwananchi ilishuhudia gari hilo dogo likiingia na kutoka uwanjani humo zaidi ya mara 10, huku watu wa msalaba mwekundu wakifanya kazi ya ziada kukusanya vijana waliokuwa hawajitambui.

Ilikuwa ngumu kumtofautisha aliyelewa kupita kiasi na aliyezimika, lakini vijana wa kiume wengi walibebwa kwenye gari ya wagonjwa kuondolewa uwanjani hapo.

Advertisement