Fally Ipupa kuwasha moto mikoa mitatu Tanzania

Saturday October 19 2019

 

By Nasra Abdallah, Mwananchi

Dar es Salaam. Msanii kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Fally Ipupa, anatarajiwa kufanya shoo katika mikoa mitatu tofauti nchini Tanzania.

Shoo hiyo aliyoipa jina la ‘World Tour 11’ kwa Tanzania ataifanya katika Mkoa  wa Arusha, Mwanza na Dar es Salaam.

Katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram,  Fally Ipupa mkali wa kibao cha Associe na Bakandja ametoa ratiba yake ya nchi tisa atakazofanya shoo kuanzia Desemba 2019 hadi Januari  2020 Tanzania ikiwemo.

Msanii huyo kwa sasa amezidi kujizolea umaarufu hapa nchini kutokana na kibao  cha ‘Inama’ alichoshirikisha na Diamond Platnumz ambacho bado kinaendelea kufanya vizuri.

Pamoja na kwamba atakwenda Uganda, Rwanda na Burundi, lakini nchini Tanzania ameonekana ndiko atakaa zaidi kwa kuwa na shoo tatu katika mikoa tofauti.

Ratiba hiyo inaonyesha kuwa Arusha atatumbuiza Desemba 18,2019 Dar es Salaam Desemba 20, 2019  huku Mwanza atatua Desemba 21, 2019.

Advertisement

Fally Ipupa kabla ya kusimama mwenyewe, awali alikuwa akifanya kazi katika bendi ya Quartier Latin  chini ya mwanamuziki, Koffie Olomide.

Tangu kujiengua huko na kusimama mwenyewe ameshapata mafanikio mbalimbali ikiwemo kuanzisha bendi na lebo yake ya muziki aliyoipa jina la F’Victeam.

Pia mwaka  2014 alishinda tuzo za AFRIMMA kama Mwanamuziki bora wa Kiume Africa ya kati, tuzo zilitolewa Jijini Dallas nchini Marekani.

Tuzo zingine alizowahi kushinda ni pamoja na ile ya mwaka 2008, kama msanii bora wa Kiume Africa kwenye ‘KORA Awards’

Mwaka 2013, alishinda tena msanii bora wa Afrika kwenye tuzo za Trace Urban Music Awards.

Advertisement