Filamu za Roma, Blank Panther, Bohemian Rhapsody, zang’ara tuzo za Oscar 2019

Tuesday February 26 2019

 

Tuzo za Oscar mwaka 2019, zimefikia kilele ambapo filamu ya Roma, Blank Panther na Bohemian Rhapsody zimeng’ara kwa kutoa washindi katika kipengele zaidi ya kimoja kati ya 24 vilivyokuwa vikiwaniwa.

Filamu ya Roma imetoa mshindi katika kipengele cha muongozaji bora, picha bora jongefu na matumizi ya lugha ya kigeni ambazo zote zilienda kwa Alfonso Cuaron.

Kwa upande wa filamu ya Blank Panther iliyochezwa na waigizaji mbalimbali akiwamo Mkenya, Lupita N’gongo, imeshinda kipengele cha muziki wa asili uliotengenezwa kwa ajili ya filamu, tuzo iliyokwenda kwa Ludwig Goransson, ambaye pia ni muandaaji wa video za muziki.

Goransson amepata tuzo hiyo ikiwa ni wiki mbili tangu atwae tuzo za muziki za Grammy, kama mtayarishaji bora kupitia wimbo wa ‘This is America’ ulioimbwa na Childish Gambino, ambao pia ulitwaa tuzo ya wimbo bora katika tuzo hizo zinazoheshimika duniani.

Filamu ya Blank Panther, pia imetoa mbunifu bora wa mavazi, tuzo iliyokwenda kwa Ruth Carter na mtayarishaji bora wa filamu iliyokwenda kwa Hannah Beachler.

Catrer na Beachler wameweka rekodi katika tuzo hizo kwa kuibuka washindi wa kwanza weusi katika vipengele walivyoshinda.

Filamu nyingine alizobuni Carter ni Amistad, Malcolm X na Selma.

Kwa upande wake Beachler, ambaye ameshiriki kutengeneza filamu ya Moonlight, Creed na kibao cha Beyonce cha Lemonade, alimshukuru mkurugenzi wa filamu ya Black Panther, Ryan Coogler na kueleza kuwa kupitia tuzo hiyo anasimama thabiti kuliko jana.

Kupitia filamu ya Bohemian Rhapsody, Alfonso Cuarón, Roma aliibuka kidedea kwenye kipengele cha picha jongefu huku ile ya mhariri wa sauti ikienda kwa John Warhurst.

Pia, filamu hiyo ilinyakua tuzo ya kipengele cha uchanganyaji muziki iliyokwenda kwa Paul Massey, Tim Cavagin na John Casali huku ya mhariri bora wa filamu ikienda kwa John Ottman.

Wengine walioshinda katika tuzo hizo, ni mwanamuziki Lady Gaga, ambaye wimbo wake ‘Shallow’ uliotumika katika filamu ya ‘A Star is Born’ ulishinda katika kipengele cha ‘Origin Song’.

Inaelezwa kuwa hiyo ni tuzo ya kwanza kwa Gaga katika maisha yake ya sanaa.

Baadhi ya vipengele vya tuzo hizo na washindi wake huku filamu zao zikiwa kwenye mabano ni:

Muigizaji bora wa kiume, Rami Malek (Bohemian Rhapsody), muigizaji bora wa kike-Olivia Colman (The Favourite), muongozaji bora, Alfonso Cuarón (Roma), filamu iliyotwaa picha bora ni Green Book.

Makala ndefu bora, Jimmy Chin na Elizabeth Chai Vasarhelyi (Free Solo) urembo na ubunifu, Greg Cannom, Kate Biscoe na Patricia Dehaney (Vice), mavazi, Ruth E. Carter (Black Panther).

Uhariri Sauti, John Warhurst (Bohemian Rhapsody), uchanganyaji muziki, Paul Massey, Tim Cavagin na John Casali (Bohemian Rhapsody).

Mhariri wa filamu, John Ottman (Bohemian Rhapsody), filamu fupi ya katuni, Domee Shi (Bao), makala fupi, Rayka Zehtabchi na Melissa Berton (End of Sentence).

Filamu fupi ya mapigano, Guy Nattiv na Jamie Ray Newman (Skin).

(Makala hii imeandaliwa na Nasra Abdallah, kwa msaada wa mitandao).

Advertisement