Harmonize kuifikisha ‘singeli’ kimataifa?

Tuesday February 11 2020

 

By Nasra Abdallah, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Msanii wa Bongo Fleva nchini Tanzania, Rajabu Abdul maarufu ‘Harmonize’ kuifikisha ‘singeli’ kimataifa?

Hilo ndio swali unaloweza kujiuliza kwa sasa baada ya msanii huyo kutia miguu kwenye muziki huo.

Mkali huyo wa kibao cha ‘Uno’ ameachia wimbo huo wa singeli alioupa jina ‘Hujanikomoa’ siku tano zilizopita  na video yake  kushika  nafasi ya kwanza kwa kuangaliwa katika mtandao wa Youtube.

Wakati audio aliachiwa siku tano zilizopita, video yake iliachiwa siku tatu zilizopita huku mwenyewe akisema lengo ni kuufikisha muziki huo nje ya Tanzania.

Huenda kuimba kwake ikawa kweli chanzo cha kuuvusha muziki huo kutokana na ukweli, Harmonize ni kati ya wasanii wanaofanya shoo katika nchi za Ulaya na Afrika kwa ujumla.

Muziki huo licha ya kupendwa na Wabongo wengi na kuimba na wasanii mbalimbali Tanzania, haujavuka boda hata katika nchi za Afrika Mashariki.

Advertisement

Muziki huo umekuwa maarufu Tanzania kutokana na kunakshiwa na ladha ya midundo ya asili, huku video zake zikiakisi maisha halisi ya wananchi wengi wa uswahilini.

Mastaa wa miondoko hiyo walitoa maoni yao ambayo yaliyonyesha imani ya muziki wao kufika mbali kwa sababu umeimbwa na  nyota huyo kutoka mkoani Mtwara.

Dulla Makabila, alisema kwa alipo Harmonize atasaidia kuukuza muziki huo.

Hata hivyo, alipoulizwa kwa nini wao wameshindwa kuupaisha, Dulla amesema, “muziki wetu umechelewa kueleweka, wanajamii bado wanauchukulia wa kihuni, ilihali ni kwa vile ulianza kutamba uswahilini kabla ya kubamba redioni na runingani,” amesema.

Mkali huyo wa wimbo ‘Hujaulamba’ amesema wanaodhani Harmonize kuingia katika miondoko hiyo atawapoteza wanakosea, badala yake atawapaisha kwani dunia itajua Tanzania tuna ladha nyingine tamu na siyo Bongofleva pekee.

Naye Mzee wa Bwax, amesema wanamkaribisha Harmonize katika miondoko hiyo  na kubainisha kuwa kitendo chake cha kuimba ni kuendelea kuupa thamani ambapo awali watu walikuwa wanachukulia kama ni muziki wa kundi fulani.

 

Advertisement