Harusi ya Lulu, Majizzo yanukia

Tuesday November 20 2018

 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi

Jana imekuwa Jumatatu nyingine ya kihistoria kwa mwigizaji Elizabeth Michael maarufu kama Lulu baada ya kutangaza rasmi kuwa anakaribia kufunga ndoa na mpenzi wake wa muda mrefu, Francis Siza au Dj Majizzo.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram aliweka picha yake akiwa na Majizzo na kuambatanisha maneno #roadtoFrancilizy akimaanisha safari ya kuelekea muungano wa Francis na Elizabeth.

Picha hiyo inawaonyesha wakiwa pamoja baada ya kumalizika kwa sherehe ya mahari.

Jana zilikuwa zimetimia siku saba kamili tangu amalize kutumikia kifungo chake cha miaka miwili baada ya mwishoni mwa mwaka jana kupatikana na hatia ya kumuua bila kukusudia aliyekuwa nguli wa filamu nchini, Steven Kanumba.

Majizzo ambaye ni Mkurugenzi wa Kituo cha televisheni na redio cha EFM, alimshtukiza Lulu kwa kumvalisha pete ya uchumba Agosti 31, mwaka huu.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram pia Majizzo aliweka picha yake na kuiambatanisha na maneno ‘Deal done’ akimaanisha ameshakamilisha kazi aliyotakiwa kuifanya siku hiyo.

Kwa Lulu inakuwa picha ya kwanza ya furaha kuweka mtandaoni kwa kipindi cha takriban mwaka mmoja.

Mara ya mwisho aliweka picha za aina hiyo Oktoba 22 mwaka jana aliposhiriki kama mgeni mwalikwa katika mahafali ya Shule ya Sekondari Kawe Ukwamani.

Lulu alikuwa akitumikia kifungo cha miaka miwili jela, baada ya Novemba 13, lakini tangu Mei 14 mwaka huu, Lulu alikuwa akitumikia kifungo cha nje kwa kufanya kazi za usafi katika ofisi za Wizara ya Mambo ya Ndani jijini Dar es Salaam.

Mwigizaji huyo mshindi wa tuzo za AMVCA alitarajiwa kumaliza adhabu yake Machi 12, mwakani lakini katika maadhimisho ya Siku ya Muungano Aprili 26, Rais John Magufuli alitoa msamaha wa kupunguza robo ya adhabu kwa baadhi ya wafungwa, naye akawa miongoni mwa wanufaika.

Advertisement