Harusi ya MC Pilipili yaiva, kiingilio Sh10,000

Saturday March 16 2019

 

By Nasra Abdallah, Mwananchi [email protected]

Mipango ya harusi ya mshereheshaji Emmanuel Mathias maarufu ‘MC Pilipili’, imepamba moto, huku ikitarajiwa baadhi ya wageni kulipia Sh10,000 ili kuhudhuria.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumamosi Machi 16, 2019, MC Pilipili ambaye pia ni mchekeshaji, amesema harusi hiyo inatarajiwa kufanyika baada ya Sikukuu ya Pasaka na itakuwa na kiingilio kitakachoanzia Sh10,000 kwa watu wa kawaida.

Amesema amefikia hatua ya kuweka kiingilio kwa kuwa hadi sasa watu wanaotaka kuhudhuria harusi hiyo ni wengi na ili kutowakosesha wengine haki ya kuiona, ameona ni bora kuweka kiingilio.

”Mpaka ninavyoongea na wewe hapa watu ni wengi sana wanaotamani siku hiyo ifike waweze kushuhudia na mimi nimeona nisiwanyime hiyo nafasi bila kujali uwezo wao kifedha, naamini kiingilio hicho kitawafaa kushiriki nasi na kusherekea siku hiyo muhimu katika maisha yetu na mke wangu mtarajiwa,” amesema.

Amefafanua zaidi kuwa hawa ni wale watakaosherehekea harusi hiyo mchana, wakati kwa wale wa usiku watakuwa na mialiko ya kadi iliyotokana na michango yao.

Pilipili alienda mbali zaidi akisema harusi yake ni ya Kitaifa, hivyo hata eneo lililopendekezwa kufanyiwa ni Uwanja wa Taifa au maegesho ya magari ya Mlimani City kwa kuwa ukumbini wameona hakutatosha.

Mshereheshaji huyo Januari mwaka huu aliibua gumzo mtandaoni baada ya kuonekana akilia wakati wa hafla ya kumvisha pete mchumba wake, Philomena Thadey.

 

Advertisement