Kesi ya Diamond Platnumz yapigwa kalenda hadi Machi 30

Muktasari:

  • Diamond Platnumz amepelekwa mahakamani kwa tuhuma za uharibifu wa mali ndani ya nyumba aliyokuwa amepanga kwa ajili ya studio maeneo ya Sinza.

Dar es Salaam. Kesi ya uharibifu wa mali inayomkabili mwanamuziki Nassibu Abdul 'Diamond Platnumz', imeahirishwa leo Machi 18, 2020 hadi Machi 30, 2020 baada ya mmoja wa wazee wa Baraza kupata udhuru.

Kesi hiyo inayosikilizwa katika Mahakama ya Ardhi Mwananyamala imeahirishwa na Hakimu Laurent Wambili kwa maelezo wazee wa Baraza wanatakiwa wawe wawili kusikiliza kesi, ila leo mmoja amepata udhuru.

Diamond Platnumz anakabiliwa na kesi ya uharibifu wa mali ndani ya nyumba pamoja na kudaiwa kodi ya mwaka mmoja.

Kesi hiyo ya madai ya vitu vyenye thamani ya Sh 33.7 milioni kwa mujibu wa wasanifu majengo waliofanya uchunguzi wa vitu vilivyoharibika ni mali ya Maulidi Wandwi.

Hata hivyo, Diamond Platnumz leo hakufika mahakamani, lakini amewakilishwa na mawakili wake Frank Modestus akisaidiwa na Gerad Hamisi.

Kwa upande wa mdai Maulidi Wandwi aliongozana na Wakili wake Felix Buruda.

Diamond Plutnumz' amepelekwa mahakamani kwa tuhuma za uharibifu wa mali ndani ya nyumba aliyokuwa amepanga kwa ajili ya studio maeneo ya Sinza Kijitonyama kabla ya kuhamia Mbezi, jijini Dar es Salaam huku akidaiwa kodi ya mwezi mmoja.

Kesi hiyo kwa mara ya kwanza ilisomwa Septemba 19, 2019 ikasomwa Septemba 24, 2019 ikasomwa Oktoba 24, 2019, Novemba 18, 2019, ilisomwa tena Januari 6, 2020 ikasomwa Februari 26 na Machi 16 mwaka huu.