Hizi ndio harakati za Hurrem Sultana, mke wa Sultan Suleiman

Wednesday June 5 2019

 

By Baraka Samson, Mwananchi

Dar es Salaam. Maeneo mengi nchini ikifika saa nne kamili wale wapenzi wa tamthilia ya Sultan wanakuwa mbele ya televisheni zao kufuatilia mfululizo wa matukio ya kusisimua.

Tamthilia hiyo inayorushwa na kituo cha televisheni cha Azam ina waigizaji wengi mahiri waliojizolea umaarufu nchini akiwemo, Hurrem Haseki Sultan ambaye kwa jina lingine anatambulika kama Roxolana.

Jina lake halisi ni Anastasia au Alexandra Lisovskaya Gavrilovna, ambaye katika tamthilia hiyo anaigiza kama kimada na baadaye mke wa Ottoman Sultan Suleiman.

Katika tamthilia hiyo, Alexandra ambaye alizaliwa mwaka 1505 katika mji wa Rohatyn, alikuwa ni mtoto wa kiongozi wa kiroho nchini Urusi  na alikamatwa akiwa na miaka 17 na kupelekwa mjini Instanbul,  Uturuki.

Binti huyu aliuzwa katika soko la watumwa na kununuliwa na Vizier Ibrahim Pasha aliyemkabidhi kwa Sultan Suleiman na kuwa kama mjakazi katika jumba lake la kifalme la Harem.

Roxolana alibadilishwa dini na kuwa muislam kisha kuingia katika familia ya kifalme ambako mamia ya wanawake walikuwa wanashikiliwa kwa ajili ya kumridhisha mfalme kingono.

Advertisement

Roxolana alibahatika kuwa mama wa watoto sita ambapo watano kati yao walikuwa wa kiume.

Katika kipindi chote baada ya kuolewa na Sultan, Alexandra alikuwa na ushawishi mkubwa kwa mumewe kuhusiana na masuala ya umma kwa ujumla, ambapo alipewa haki ya kupokea mabalozi na kuishi maisha kama mke halali wa mtawala wa Ottoman

Hürrem Sultana, ambaye chanzo cha kifo chake hakujulikani alifariki mwaka 1558 na kuzikwa katika kaburi lenye thamani katika makaburi ya familia ya Sultan.

Mama huyu anaaminika kuwa mwanamke katili aliyefanikiwa kuwaondoa kwa nguvu zote watu wote aliowachukia, huku maisha yake yote yakitawaliwa na jitihada za kufanya apendwe na Sultan, hali iliyopelekea mfalme huyo kuwa tayari kufanya chochote kile kwa ajili yake.

Kuna visa kadhaa vya kukumbukwa, hasa Hurrem alivyokuwa akipambana na kila mwanamke aliyekuwa na uhusiano na Suleiman na haikuwa ajabu kuona akijaribu kuwatoa uhai wanawake hao.

Kila aliyekuwa akitaka kuteka akili za Suleiman, wakiwemo ndugu wa mfalme huyo waligeuka maadui wa Hurrem.

Pia mwanamke huyo alipambana kuwaweka sawa watoto wake Beazil na Selin waliokuwa na uhasama huku kila mmoja akitaka kumuua mwenzake ili kurithi kiti cha ufalme kutoka kwa baba yao, Suleiman.

Advertisement