NO AGENDA: Huyu Lady Jaydee ni komando hadi chenji inabaki

SAFIRI kutoka mwaka 2000 mpaka 2020. Ni kweli bana! Miaka 20 imetimia. Da Jide hajatuongopea. Anakwenda kusherehekea miaka yake 20 ya kuihudumia game ya Bongo Fleva.

Mpate katika masafa ya Lady Jaydee. Ukimsaka kwa frequency za Binti Komando pia anasomeka. Kuna kipindi alipenda kujiliza, halafu akajiita Binti Machozi, eti siku hizi hapendi hilo jina. Hata ile chaneli yake ya Mama Somefood hainasi tena. Ukibonyeza passport yake utakuta utambulisho aliopewa na wazazi wake, Judith Wambura Mbibo. Kama nasikiliza ile ngoma yake “Machozi”, ile sauti kama inanidekea, “nailazimisha furaha, lakini moyoni nina majonzi”, wavimba macho wakadhani kweli Jide ni cha kudeka na mwepesi kumwaga ‘mchozi’, weeee! Jide ni mwanamke na chenji inarudi.

Kipindi ambacho game ilitawaliwa na masela. Wahuni wanaorap wakiteka mawimbi. Jaydee alifanya kila kitu kiwezekane na ghafla akawa ndiye malkia wa Bongo Fleva. Yes, Jide ni godmother wa huu muziki ambao madogo wengi wanautambia. Jide ni pioneer. Unaweza kudhani ni juzi, Jaydee alipotoa albamu ya “Machozi”, kisha “Binti” halafu akawasha “Moto”. Wakati kwenye machozi alilia, kwenye Binti alifanya kila kitu kumhamasisha mtoto wa kike na wanawake kwa jumla, kujitambua na kutobweteka. In short, aliwapa sana za chembe wanaume.

Sitamsahau Jaydee alivyoamua kuifanya issue ya wanaume kulelewa na mamanzi wao kuwa ni kesi endelevu. Akaingia booth na MwanaFA, akatoa kitu “Wanaume Kama Mabinti”, akaona dawa haijakolea, akarudi booth na Papii Kocha, wakaifanza remix kiroho mbaya.

Sikumhusudu Jide alipoamua kuwasanua wanawake kwa wimbo “Usiusemee Moyo”. Aliwakalisha kitako, eti wasizubae kutupenda akina sisi minjemba. Eti kuna mengi huyafanya tunapokuwa mbali nao. Jide alitema sana sumu ndani ya Binti. Hata hivyo, Siri Yangu ni ngoma ya Jide niliyoikubali kuliko zote ndani ya Binti.

Mzigo wa Lady Jaydee “Nessun Problema” au wengi waliutambua kwa jina la “Nakupenda” ambao Terry ‘Fanani’ wa HBC alitambaa na mimbembelezo ya kigumu, hiyo ndio ngoma yangu tamu ya muda wote kutoka kwa Jide!

Kisha, Jaydee badala ya kuzingatia jinsi mgumu Fanani alivyobembeleza, akampa mikausho “stori nyingi za nini? Acha mapozi, weka utoto pembeni. Kama unanipenda mbona shega tu. Dini, lugha sio kikwazo, mradi nyoyo zinaelewana.” Nessun Problema. Ndio, hakuna tatizo. Sema nini? Kwenye Machozi, Jaydee alijiliza sana. Alikosa wa kuwalilia mpaka akaenda kuyamwaga machozi kwa mhuni wa Temeke, Sir Nature Kiroboto. Akamwambia alikuwa akiona “Umuhimu” wake. Ni baada ya Nature kusepa zake. Katika Machozi Jaydee mnyonge, kwenye Binti akawa mbabe huyo, kisha akawasha “Moto”.

Jaydee ni muziki, ni ladha. Jaydee ni maisha, ni shule. Jaydee yumo ndani ya historia ya sanaa Tanzania. Vyovyote vile, utakapoizungumza historia ya Tanzania na ukuaji wa sekta zake, Jaydee ni historia ya muziki na burudani. Ndio, Jaydee ni historia ya Tanzania.

Unaweza kuona kama juzi vile, kumbe tayari miaka 20 imeenea. Sometimes kunakupwa lakini jua halizami kabla ya kujaa. Uzuri alishatutanabahisha kuwa “Siku Hazigandi”. Jaydee ametoa huduma ya muziki kama vile hakukuwa na mwingine kabla na hayupo baada yake.

Muziki na mtokeo yake. Pesa zikaingia na kila mtu akaona Jaydee maisha kwake ni super. Unauliza magari ya kifahari? Toka kusukuma Escudo, halafu akakokota Prado. Mtalaka wake, Gardner Habash alipokula mzinga na Prado, Jaydee akavuta Mitsubishi Pajero. Kama vile kukata mti na kupanda mwingine. Jaydee kubadili magari ni kama demu mdangaji anavyobadili mavazi ayavutie madanga. Au mlevi all weather anavyohama pombe kulingana na kipato au mazingira. Leo K-Vant, kesho Konyagi, juzi Heineken, jana alijisajili na Kilimanjaro. Katikati ya mwezi Balimi, mwisho wa mwezi anafyonza Absolute. Ndivyo Jaydee na magari. Baadaye mitoko yake ikategemea Nissan Murano. Sijui unanimanya?

Mara akasukuma gari la kifahari sana. Full umeme. Range Rover Evoque. Kibongo Bongo, hakuna mwanamuziki wa kike ambaye muziki umemtendea heri nyingi kama Lady Jaydee. Mlete wako halafu nikupige naye masingi muondoke mnasaidiana kulia.

Machozi Band ikawa biashara inayolipa. Kila weekend people zilijazana pale Nyumbani Lounge, Namanga, kupata huduma ya Mama Somefood na timu yake. Unakula, unakunywa na muziki mzuri unahudumiwa.

Tukawa hatuwaoni maofisa wa Machozi Band kwenye daladala. Bendi ilikuwa na magari. Ungeyatambua kwa yale machata ya Machozi Band. Nikiwa nasimulia habari za Jaydee, tafuta wa kubishana naye. Mimi huniwezi. Haki nakuapia!

Safari haikosi changamoto. Skendo zikawepo. Wakaja wanamuziki wakapimwa naye. Unique Sisters walipita. Stara Thomas alipewa nafasi yake. Ray C akatambulishwa ndiye kiboko ya Jide. Renee sijui alipotelea wapi, Hafsa Kazinja naye? Waite wote. Jaydee alibaki solid, tena with head high!

Ni rahisi kubishana kuhusu mwanamuziki bora wa kiume wa muda wote katika Bongo Fleva, lakini kwa wanawake msilete ‘maujinga’ yenu. Wengine wote wanaruhusiwa kugombea namba mbili, tatu, nne na kuendelea. Namba moja Jaydee hashindanishwi na yeyote. Mimi ndio jaji mkuu wa haya makitu. Na hii ndio final judgement.

Mbabe kwenye booth, mtemi akiwa jukwaani na live band. Akili ‘mingi’, akiwa anahojiwa anajua amnyime interviewer jibu gani na ampe lipi. Hatoshelezi tu vigezo vya kuwa chemli ya kila mwanamke kwenye giza la muziki na sanaa kwa jumla, bali ni karabai la kimaisha kwa wanawake, hasa waliozingirwa na giza la ukandamizaji. Mjaribu Jide, kisha utamwona anavyogeuka joka kubwa, mithili ya Anaconda msituni Amazon.

Hatufukui makaburi somo, ila tunasahau vipi lile sokomoko la baada ya Joto Hasira? Jaydee aliweza kuufanya uwanja wa mapambano uwe tambarare dhidi ya most powerful men kwenye mzingo wa burudani Bongoland. Nani alishinda? Kwangu sio big deal. Muhimu ni uthubutu na ujasiri wa Jaydee nyuma ya kichuri alicholishwa Ukuryani?

Unadhani Jaydee ni malaika? Ana dhambi kibao. Kinachombeba ni kujitambua kwake halafu anajiheshimu. Mwanamke mtegemea wanaume? Huko humkuti. Kila siku na mishemishe kutengeneza tembo wekundu na benjamins za Wamarekani.

Miaka 20 ya Jaydee inanihusu sana. Inakuhusu wewe. Inamhusu kila mtu Afrika Mashariki. Lazima kumwonesha kuwa sisi wateja wake ndani ya miaka yake 20 ya huduma, ni wenye shukurani na tunamheshimu. Sema Royal Village, Dodoma ni padogo. Hapakidhi heshima ya Lady Jaydee ya utoaji huduma kwa miaka 20. Shoo ya hivyo inafaa stadium. Kama vipi akifanya Dar iwe Uwanja wa Taifa ikipungua Uwanja wa Uhuru. Period!

Ni Februari Mosi sio? Wewe utapenda Yahaya au Distance? I Am au Mawazo? Teja au Upo Juu? Acha kuchosha ubongo kuwaza nyimbo za Jaydee. Yule ni Mom In Chief wa Bongo Fleva, kwa hiyo package yake ni heavy-duty.