JB awashukia wasanii wa Tanzania

Muktasari:

Msanii wa filamu nchini Tanzania, Jacob Steven maarufu JB amewakosoa baadhi ya wasanii kubadili mwonekano wa watoto wao ili kuvutia zaidi na kuweka picha zao kwenye mitandao ya kijamii.


Dar es Salaam. Msanii wa filamu nchini Tanzania, Jacob Steven maarufu JB amewakosoa baadhi ya wasanii kubadili mwonekano wa watoto wao ili kuvutia zaidi na kuweka picha zao kwenye mitandao ya kijamii.

Ametoa kauli hiyo leo Jumatano Novemba 27, 2019 katika mkutano na waandishi wa habari wakati akizungumzia kongamano la amani la familia litakalofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Novemba 30, 2019.

Amsema amani katika familia inatia shaka kutokana na mmomonyoko wa maadili kwa maelezo kuwa  baadhi ya wazazi wanawabadili watoto wao mwonekano kwa kuwapaka vitu mbalimbali ili wavutie.

"Zamani tulipokuwa tunasoma tulitamani kuwaiga waliokuwa wakifanya vyema darasani, lakini kizazi cha sasa mtoto  anatamani kuwa na  mwonekano mzuri kama wa mtoto wa fulani jambo ambalo si zuri katika makuzi ya watoto wetu na familia kwa ujumla.”

"Hivyo kuja kwa kongamano hili najua familia zitajifunza mengi na ninafurahi kuwa mmoja wa mabalozi ambao nitawasaidia kuisambaza elimu inayohusu masuala ya familia,” amesema JB.

Msanii mwingine wa filamu, Rose Ndauka amesema wasanii wana nafasi kubwa katika jamii ikiwa ni pamoja na kuelimisha na kuburudisha, “tutatumia nafasi kutoa elimu kwa vijana ili waje kuwa viongozi bora na wazazi wenye maadili hapo baadaye.”

Awali,  kiongozi wa shirikisho la taasisi za amani nchini Tanzania, Stylos Simbamwene amesema katika kongamano hilo kuwakuwa na washiriki mbalimbali wakiwemo wabunge na viongozi wa asasi mbalimbali.