Kiba jukwaani saa tatu kwa nguo tano tofauti

Sunday December 30 2018

 

By Nasra Abdallah,Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Katika suala la nguo, Ali Kiba ni habari nyingine, kwani katika shoo yake ya ‘Funga mwaka na AliKiba’ alitumia saa tatu jukwaani huku akibadili mavazi matano tofauti.

Shoo ya Ali Kiba ilifanyika jana Jumamosi katika Ukumbi wa Next Door Arena na kusindikizwa na wasanii mbalimbali akiwemo Mwana FA, Nuhu Mziwanda, Barnaba, The Mafik, Bilnas, Aslay, The Kings Music, Papii Kocha na Mr Blue.

Pamoja na kulitumia jukwaa kwa saa tatu, alibadili nguo mara nne  kwa wakati huo mfupi huku zote zikibamba vilivyo.

Awali, wakati anafika ukumbini hapo majira ya saa 5:30, Kiba alikuwa amevaa suti ambayo koti lake alilishika mkononi, huku akibaki na kizibao na shati jeupe.

Ilipofika saa ya kupanda jukwaani majira ya 6:30 usiku, alivaa fulana nyeusi mithili ya yenye nyuzinyuzi na suruali nyeusi huku sehemu kubwa ya boxer yake nyeupe ikiwa inaonekana.

Shati la mtelezo la maruni na suruali nyeusi, huku chini akiwa amevalia viatu vya maruni, alipanda na viwalo hivyo wakati anaimba na wasanii wake wa Kings Music.

Aliporudi mara ya tatu Kiba alibadili kitu kingine kwa kuvaa kaptura na shati lenye rangi za African Print, nguo ambazo zilimuonyesha mwanaume wa kiafrika haswa.

Katika kumalizia shoo, alibadili na kuvaa kizibao cheusi ambacho hakufunga vifungo kilichokuwa kimechanganyia na rangi ya gold.

Mbunifu wa mavazi hayo yote, Noel Ndale, ambaye amekuwa akimvisha Kiba kwa muda mrefu sasa, amesema msanii huyo amekuwa akipenda nguo ambazo hazina mambo mengi.

 

Advertisement