King Kiba aeleza alivyokatishwa tamaa na Mr Blue

Msanii anayefanya vizuri katika muziki wa Bongo Fleva, Ali Kiba au King Kiba, amesema wakati anataka kuingia kwenye muziki, msanii mwenzake Khery Sameer ‘Mr Blue’ alionyesha kumkatisha tamaa kwa kumwambia muziki sio masihara.

Ali Kiba aliyasema hayo mwishoni mwa wiki katika shoo yake ya ‘Fungamwaka na AliKiba’, iliyofanyika katika Ukumbi wa Next Door Arena.

Pamoja na kauli hiyo alisema hakukata tamaa bali alijitahidi kuwa karibu na wasanii wa bongo fleva hususan Mr Blue na Abby Skills kila wakati wakiwa wanafanya kazi zao za muziki.

“Nilipokuwa nikiwaangalia huku nikiwa tayari nina kauntabuku nyumbani limejaa mashairi na kati ya yake ulikuwamo wimbo wa Maria ambao niliwaandikia ili wauimbe (Mr Blue na Abby Skills).

“Baada ya kuusikiliza, Blue alitaka na mimi niwe mmoja wa waimbaji katika wimbo huo na hapo ndio ukawa mwanzo wangu wa kutoboa mpaka mnavyoniona hii leo,” alibainisha Kiba ambaye kwa sasa anatesa na wimbo wa Kadogo.

Akielezea kuhusu shoo yake, alisema anashukuru kwa namna watu walivyojitokeza na kuahidi kuwa kila mwisho wa mwaka atajitahidi kuufunga na mashabiki kwa namna hiyo.

Katika shoo hiyo Ali Kiba alipanda jukwaani saa 7.00 usiku na kuanza kuporomosha nyimbo zake za zamani na za sasa.

Kati ya hizo ni mapenzi yana-run dunia, Cinderella, Aje, Mvumo wa Radi huku akifunga shoo hiyo 9.30 usiku na kibao cha Seduce Me.

Kwa upande wa wasanii waliomsindikiza mbali na Mr Blue ambaye aliwakosha mashabiki alipoimba wimbo wa ‘Mboga Saba’ ambao Kiba aliutendea haki katika kiitikio, alikuwepo Nuh Mziwanda ambaye walikinukisha naye wimbo wa Jike Shupa na kuibua shangwe katika ukumbi huo.

Wasanii wengine ni Papii Kocha, Dogo Aslay, MwanaFA, Barnaba, The Mafik, Bilnas na The Kings Music.