Kolabo za nje zinavyombeba Diamond Platnumz kimataifa

Muktasari:

Nyimbo za msanii wa Tanzania, Diamond Platnumz zinazopata watazamaji wengi katika mtandao wa Youtube ni zile alizowashirikisha wasanii wa nje ya Tanzania.

Dar es Salaam. Msanii Diamond Platnumz ambaye jina lake linazidi kuwa kubwa kimataifa na amekuwa na mafanikio makubwa katika muziki wake toka ameingia kwenye tasnia ya muziki.

Diamond amezidi kujipatia umaarufu na thamani yake kuongezeka zaidi anaposhirikiana na wazanii wa mataifa mengine katika muziki wake.

Nyimbo za msanii wa Tanzania, Diamond Platnumz zinazofanya vizuri katika mtandao wa Youtube ni zile alizowashirikisha wasanii mbalimbali wa nje ya Tanzania.

Diamond ambaye jina lake halisi ni Nassib Abdul hadi jana Machi 23, 2020 ameshafikisha watazamaji zaidi ya milioni 900 kwenye mtandao huo na kuwaacha mbali wasanii wengine wa Afrika wanaofanya vizuri katika tasnia ya muziki akiwemo Wizkid, Davido na Burnaboy.

Licha ya kuwa na watazamaji wengi, Diamond ana nyimbo tano zinazoongoza kwa kutazamwa katika mtandao huo, zote ni alizowashirikisha wasanii hao.

 

Nyimbo ya kwanza inayoongoza kwa kutazamwa mara nyingi  ni Yope Remix aliyoimba na msanii Enoss B ambaye ni raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC). Wimbo huo umetazamwa mara milioni 73.

Wimbo mwingine ni Nana aliyoimba na msanii  Mr Flavour wa Nigeria ambao umetazamwa mara milioni 60.

Wimbo wa Inama alioimba na Fally Ipupa ambaye ni raia wa DRC umetazamwa mara milioni 52.

Wimbo African Beauty aliomshirikisha msanii wa Marekani, Omarion umekamata namba nne kwa kutazamwa mara milioni 45 huku ule wa Marry you alioimba na Neyo ukitazamwa mara milioni 41.

Tangu ameanza muziki miaka 10 iliyopita, Diamond mwenye umri wa miaka 31 ameimba nyimbo mbalimbali zikiwemo Kamwambie, Mbagala, Mawazo, Lala Salama, Mdogo mdogo, Nitampata wapi, Utanipenda’, Eneka, Baila, Kanyaga, Baba Lao, I Miss You, The One na Jeje.