Lugha tatizo Sauti ya Busara

Kundi la Swahili Encounters wakitoa burudani kwenye tamasha la sauti za busara 2020 Visiwani Zanzibar eneo la Ngome Kongwe

Muktasari:

  • Swahili Encounters waeleza changamoto ya kuimba wimbo wa pamoja  katika  Tamasha  la sauti za  Busara

KUNDI la Swahili Encounters linaloundwa na wasanii kutoka Zanzibar, Moroco, Ghana, Uingereza, Tanzania, Algeria na kuimba wimbo wa pamoja wamesema lugha ni changamoto wanayopata katika ushiriki wa kuimba kwa pamoja.

Wanamuziki hao huwa wanakutana  siku tatu kabla ya Tamasha la Sauti za Busara  kuanza linalofanyika Mji Mkongwe, Ngome Kongwe kisiwani hapa, hutanga wimbo mmoja unaohamasisha kauli mbiu ya tamasha hilo.

Wamesema changamoto wanayokutana nayo ni kwa kuwa wanakutana nchi nyingi, hivyo inachukua muda kuelewana hadi kukamilika wimbo.

Amina Omary maarufu Siti Amina  kutoka Tanzania amesema kwakuwa muziki pekee yake ni lugha na hisia hivyo hutumia mbinu hiyo kukamilisha wimbo wa pamoja kutoka kila nchi.

“Ukweli hadi wimbo kukamilika huwa tunapata wakati mgumu sana kwa kuelewana sisi waimbaji, ila kwakuwa muziki ni hisia na ni lugha basi tunatumia njia hiyo kuelewana na kutoa kitu kizuri” alisema Sitti

Naye mwanamuziki Mehdi Laifaoui kutoka Algeria amesema kutoelewana lugha katika kushiriki kuimba wimbo wa pamoja kumesababisha  mwaka huu kuwa na mwongozaji anayejua lugha za nchi tofauti tofauti  ili kuwasaidia kuelewana.

“Kuna ugumu tunaoupata katika kutunga nyimbo ya pamoja kama unavyoona tunakutana nchi tofauti tofauti , uzuri mwaka huu tumepata  muongozaji  wa nchini tofauti  na mwisho wa siku kukaa pamoja na kuelewana” alisema Mehdi

Kundi hilo la Swahili Encounters ambalo huwa linaundwa kipindi cha tamasha hilo huvunjika mwisho wa tamasha, wamesema huwa kila mwanamuziki mmoja anatunga kipande chake cha shairi na baada ya hapo huunganisha na kutoa wimbo kamili na mwaka huu wametoa wimbo unaoitwa ‘Sisi ni Sawa’ ambao unazungumzia kauli mbiu ya  tamasha hili  inayosema  ni  Paza Sauti, pinga unyanyasaji wa kijinsia.