Lulu aanza kukutana na mashabiki wake

Tuesday January 22 2019

 

By Nasra Abdallah, Mwananchi [email protected]

Msanii wa filamu, Elizabeth Michael maarufu kwa jina la Lulu, ameanza kuzungumza na mashabiki wake juu ya mambo mbalimbali ikiwamo kuwaweka wazi ni lini ataanza kugawa nguo zake ambazo waliwahi kuzipenda walipomuona akiwa amezivaa.

Lulu anawasiliana na mashabiki wake ikiwa imepita miezi miwili tangu alipomaliza kutumikia adhabu ya kifungo baada ya kutiwa hatiani kwa kumuuua bila ya kukusudia, aliyekuwa mpenzi wake, Steven Kanumba, na baadaye kubadilishiwa kifungo hicho kuwa cha nje kwa kufanya shughuli mbalimbali katika ofisi za Wizara ya Mambo ya Ndani hadi Novemba 12, mwaka jana alipomaliza adhabu hiyo.

Ingawa alikuwa akitumikia kifungo cha nje, Lulu hakuwahi kujibu chochote katika mtandao wake zaidi ya kutupia picha, ikiwamo ile ya kumtakia heri ya siku ya kuzaliwa mchumba wake Francis Ciza ‘Majizo’, Septemba 9, mwaka jana.

Baada ya hapo alikuwa akiweka katika mtandao wake vitu mbalimbali ikiwamo Novemba 16, alipoandika maneno ya kuwashukuru wote waliomuombea wakati akitumikia kifungo.

Hata hivyo, licha ya muda wote huo mashabiki wake kumpa hongera na kumwandikia ujumbe mbalimbali, hajawahi kujibu chochote bali alikuwa akitupia picha na kuandika maneno mafupi.

Juzi, kwa mara ya kwanza msanii huyo aliyewahi kutesa na filamu mbalimbali ikiwamo ya Family Tears, Family Disater na Foolish Age, alijibu maswali mbalimbali ya mashabiki alipowapa fursa ya kumuuliza chochote ambacho wangependa ajibu.

Mojawapo ya maswali aliyoyajibu ni kutoka kwa Kidohty aliyemuuliza ’Dada yangu unazidi kuwa mzuri nini siri. Katika majibu yake Lulu alijibu kwa kifupi kuwa ni ‘Damu ya Yesu Baba.’

Swali lingine ni lile lililotoka kwa Uswahili_tz aliyemkumbusha kuhusu nguo alizotangaza kuzigawa kwa waliopendezwa nazo wamuonapo akiwa amezivaa.

Uswahili aliandika “Sasa vipi ile ishu ya kugawa nguo, wengine tushakopa na kupanga maduka ugawe hizo nguo tuuze mitumba aisee”. Katika hilo, Lulu alijibu atafanya hivyo siku za karibuni na kuomba radhi kwa kuchelewa.

Naye Alpher Emmanuel alimuuliza kama alishawahi kusoma Shule ya Msingi Hekima ambapo alimjibu ni kweli, lakini Buguruni B, kwani ukweli ni kuwa shule zote hizo zipo eneo moja Buguruni Chama.

Mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Irene Nancy, alimuuliza kuhusu urembo unaoonekana katika meno kupitia picha aliyoiweka wakati akijibu maswali ya mashabiki wake na kuongeza kuwa huenda kinadada wa mjini wakaanza kumuiga, ambapo naye alimjibu kuwa hiyo ni dawa.

Advertisement