Lupita Nyong’o: Kumtambulisha mtu kwa rangi yake ni ubaguzi

Muktasari:

Mshindi wa tuzo ya Oscar Lupita Nyong’o ameliambia Shirika la Utangazaji Uingereza (BBC) kuwa wanaowabagua watu weusi ni weusi wenyewe, kulifananisha jambo hilo na ukoloni wa ubaguzi wa rangi.

Mshindi wa tuzo ya Oscar Lupita Nyong’o ameliambia Shirika la Utangazaji Uingereza (BBC) kuwa wanaowabagua watu weusi ni weusi wenyewe, kulifananisha jambo hilo na ukoloni wa ubaguzi wa rangi.

Amesema jambo hilo bado linaitafuna dunia  kwa maelezo kuwa bado wana wanatambulishana, “huyu mweusi, yule mweupe.”

“Kumtambua mtu kwa rangi yake ni mwanzo wa ubaguzi wa rangi. Inasikitisha  haya yanatokea katika nchi zetu ambapo wengi zaidi ni weusi, kuliko weupe.”

Nyong’o aliyezaliwa Kenya na kuhamia nchini Marekani amesema kuwa ngozi nyeusi ilimfanya ajione hana thamani.

“Nimekuwa wa thamani nikiwa na ngozi hii nyeusi, lakini tangu nakuwa nilikuwa najiona sina thamani baada ya mdogo wangu aliyekuwa mweupe kuitwa mrembo, ”amesema Lupita.

Amesema kuwa ubaguzi huo wa rangi hautakwisha kama weusi hawataamua kuona watu wote ni sawa na rangi ya ngozi haibadili chochote kwa yeyote.