Maajabu ya wasanii wa Wasafi kubaniwa tamasha la Wasafi

MJINI pamechangamka, mitandao ipo moto. Vipi tena Ebitoke na Mlela? Twitter kuna Gigy Money feki anajitafutia kiki kupitia Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamis Kigwangalla. Kuhusu Wasafi Festival na mengine, ma-MP wa kitaa, Luqman Maloto na Dk Levy wanaweka kila kitu kweupe.

LUQMAN: Umesikia kuwa zimepigwa kati ya Ebitoke na Yusuf Mlela?

DK LEVY: Ebitoke ndio madudu gani? Umeniacha mbaaali! Hilo neno nimelifananisha na ndizi, si unajua pande za Kashai ndizi zinaitwa matoke? Au Ebitoke ni matoke yaliyoungua?

LUQMAN: Nimekosea, Ebitoke amechapana na demu wa Mlela, eti wanamgombea Mlela.

DK LEVY: Tatizo lako ukishavuta ugoro unakuwa mgumu wa kujibu maswali. Ebitoke ndio nani? Mlela namjua alikuwa msanii, kwani siku hizi anafanya biashara ya kupika na kuuza matoke?

LUQMAN: Jiheshimu, nani mvuta ugoro?

DK LEVY: Tubishane ugoro kwanza au utanijibu swali ili tujadili hoja mezani?

LUQMAN: Unajitoa ufahamu sana, wewe ni wa kumtojua mchekeshaji wako pendwa Ebitoke? Na kwani hujui kuwa kilipita kipindi Mlela na Ebitoke walikuwa ‘capo’ gumzo mitandaoni?

DK LEVY: Umesema vizuri kuwa ilikuwa ‘capo’ gumzo kwenye mitandao. Kwa hiyo sio dunia halisi yenye uhalisia ambayo naishi mimi na watu wengine halisi. Na unajua mimi dunia ya mitandao huwa naitazama kwa darubini. Na darubini yangu haijawahi kumwona mtu anaiyeitwa Ebitoke, ndio maana uliponitajia hilo jina nilidhani ni matoke yaliyoungua.

Enewei, sio kesi. Sasa kama ni watu wa mitandao na mapenzi yao ni ya mitandao, kuwajadili ni kupoteza muda. Ukifuatilia utakuta hakuna ugomvi wa mapenzi, ila wameamua kuchonga kiki. Sisi wakati tunajadili ugomvi wao, wenyewe wanapongezana kwa igizo zuri la kugombana. Achana nao. Ukitaka tugombane niulize swali lingine kuhusu hao raia.

LUQMAN: Basi nisamehe, naapa sitarudia. Vipi shoo ya Wasafi Festival? Uliona pengo lolote?

DK LEVY: Unaulizia pengo la Konde Boy, Ali Kiba au penseli?

LUQMAN: Achana na hao wasiohusika na shoo. Tujadili tamasha lilivyofanyika.

DK LEVY: Naachana nao kivipi wakati kuelekea hilo tamasha majina maarufu yaliyotajwa yalikuwa ya hao watatu, Konde Boy, Ali Kiba na penseli, kuliko waliotakiwa kufaya shoo? Hivi huwa unatumia chumba kipi cha ubongo kufikiri? Usije ukawa unatumia chumba cha kubadilishia nguo.

LUQMAN: Wewe ndiye mvuta ugoro sasa, unataka tuwajadili watu ambao hawakuhusika na shoo, wakati mzigo ulifanyika bila wao.

DK LEVY: Wewe jamaa kuna wakati kukaa na wewe kikao kimoja huwa napata shida. Umeniuliza pengo unataka nikujibu nini zaidi ya kukutajia watu ambao hawakuwepo? Haya nijibu wewe, uliona pengo gani Wasafi Festival?

LUQMAN: Swali zuri Daktari. Wasafi Festival ilikuwa shoo yenye wasanii wakali lakini haikuandaliwa vizuri, kwa hiyo iliishia kuwa na mizuka ya mgawo, watu washangilie, muda mwingine ikawa kama watu wapo msibani.

DK LEVY: Hilo haliwezi kuwa tatizo la waandaaji. Akipanda jukwaani msanii mkali lazima nyomi liitike, lakini akifuata mbovu uwanja utazizima ziii kama msibani. Jifunze kuelewa makosa na kuyaelekeza kwa walengwa. Usiwabebeshe lawama waandaaji makosa ya wasanii wachovu walioshindwa kuamsha.

LUQMAN: Inaonekana najadiliana na mtu ambaye hakuwepo kwenye tamasha. Shoo ya Wasafi ilikuwa ya mafungu mno. Haikuwa na ratiba inayosomeka na kueleweka. Stori nyingi kwenye shoo ya burudani usiku. Ghafla Wasafi Festival likageuka jukwaa la siasa na matangazo mengi mpaka raia wakaona kero. Wewe unajua mawaidha kwenye ‘party’ ni tendo la dhambi.

Kuna wakati, tena sio mara moja, jukwaa lilibaki tupu karibu dakika 10 nzima, mpaka unajiuliza ina maana wakati wanatangaza watu waende hawakuwa wamejipanga? Uandaaji wa matamasha na upangaji wa ratiba yenye kuburudisha ni aina nyingine ya kipaji. Ratiba ya Wasafi Festival ilikuwa ya hovyo kuwahi kushuhudia, ingawa kulikuwa na wasanii wakali sana. Una swali kabla sijaendelea?

DK LEVY: Acha kujishitukia, mimi nakusikiliza halafu wewe unatamani nikuulize. Hebu endelea.

LIQMAN: Mbali na ratiba kuwa shaghala baghala, vilevile ma-MC nao walikuwa chini ya kiwango. Yule Jonijo na Ray walizidiwa sana na ukubwa wa shughuli. Walipoooa, hawakuchangamsha. Walikuwa baridii (kwa sauti ya JK). Kuna mambo mengi ambayo Wasafi wanatakiwa kujifunza ili kufanya matamasha yao. Unaweza kuwa na wasanii wakali lakini shoo ikawa mbovu na watu wakaondoka wamenuna. Hujui hilo?

DK LEVY: Wewe mbona unataka kila kitu unachokifikifikiria wewe ukijazie pointi kutoka kwangu? Wewe Mwinyi Zahera nini?

LUQMAN: Na wewe Antonio Nugaz nini? Hata kama hutaki maswali nakuuliza utake usitake. Hivi Wasafi Festival msingi wake ni shoo ya wasanii kutoka Wasafi au wageni?

DK LEVY: Mbona hilo jibu lipo ‘streiti’ kama ugomvi na konda ukimpa noti ya Sh10,000 asubuhi? Ile ni shoo ya Wasafi, kwa hiyo wasanii kutoka Wasafi ndio wanatakiwa kuonekana zaidi kuliko waalikwa. Siku zote mwenye shoo anatakiwa na anatarajiwa kupiga mzigo kuliko waalikwa. Huwezi kuzindua albamu, halafu unaowaalika wakusindikize wapige shoo kali na ya muda mrefu kuliko mwenye albamu. Ikiwa hivyo, basi shoo itakuwa imebakwa, sorry, namaanisha imetekwa.

LUQMAN: Wageni walipewa muda mrefu kupiga shoo kuliko wenyeji. Wale watoto Rayvanny na Mbosso waliimba nyimbo mbilimbili tu, wakati lile ndio lilikuwa jukwaa lao la kujimwambafai. Shida sio wasanii waalikwa walipendelewa, ukweli muda mwingi ulipotea bila mpango kutokana na ratiba yao ya hovyo. Wangepangilia vizuri, Rayvanny asingekosa muda wa kutosha au Mbosso. Shoo ya Wasafi kuwabania wasanii wa Wasafi, ni kituko cha mwaka.

DK LEVY: Kumbe kila kitu unakijua, badala ya kuweka msosi mezani tule, unaanza kuniuliza ‘una njaa?’ Mara ooh ‘umeshakula?’ Ungesema moja kwa moja kuwa wasanii wa Wasafi walipunjwa

LUQMAN: Je, yule anayejiita Gigy Money, alivyoamua kumshambulia Kigwangalla kuwa ana siri zake DM kule Twitter, huyo unamzungumziaje?

DK LEVY: Kati ya binadamu huwa nawaamini sana ni Kigwangalla. Najua atamalizana naye inavyotakiwa. Sina wasiwasi naye. Tumpe muda!