Makonda: Asiyetambua mchango wa Ruge kwenye muziki akapimwe akili

Muktasari:

  • Mkurugenzi huyo wa Vipindi wa Clouds FM = anaendelea kupatiwa matibabu Afrika Kusini kutokana na maradhi yanayomsumbua ambapo ametimiza miezi kadhaa tangu alipokwenda nchini humo.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, amesema mtu ambaye hatambui mchango wa Ruge Mutahaba katika kuendeleza muziki wa kizazi kipya, akapimwe akili hospitali ya Milembe mkoani Dodoma.

Makonda aliyasema hayo usiku wa kuamkia jana, aliposhiriki tamasha la Fiesta lililofanyika kwenye viwanja vya Posta, Kijitonyama, Dar es Salaam.

Makonda aliyetia timu katika tamasha hilo saa 7.00 usiku, alisema mchango wa Ruge ambaye ni mkurugenzi wa vipindi wa kampuni ya Clouds Media katika tasnia ya muziki hakuna asiyeujua na kuwaomba Watanzania kuendelea kumwombea ili apone na kurejea kwenye majukumu yake.

Ruge kwa sasa anaendelea kupatiwa matibabu Afrika Kusini kutokana na maradhi yanayomsumbua ambapo ametimiza miezi kadhaa tangu alipokwenda nchini humo.

Makonda alipingana na watu wanaodai kuwa mkurugenzi huyo amekuwa mmoja wa watu wanaowabania wasanii.

“Wanaosema hivyo wanapaswa kuelewa kuwa siku zote kama kuna mtu aliyekubania katika maisha basi mafanikio uliyonayo ni kwa sababu yake.

“Katika maisha unapaswa kumshukuru mtu aliyewahi kukubania badala ya kumlaumu kwa kuwa amekuwa chachu ya mafanikio yako. Kuna watu walinyanyaswa na wazazi au walezi wao, lakini leo wana fedha zao na wamejilipia kiingilio kuja kuiona Fiesta, kweli si kweli?” Alihoji Makonda huku watu wakiitikia kwa shangwe kweliii!

Pia, katika usiku huo, Makonda aliuongoza umati wa watu waliohudhuria Fiesta kumuombea Ruge na hii ni baada ya kumaliza kuangalia video iliyomuonyesha akieleza namna alivyo na ndoto ya kuendeleza vijana na muziki wa hapa nchini.

Makonda aliongoza maombi ili Mungu amrudishe Ruge nchini akiwa na hali nzuri kiafya ambapo umati uliokuwapo viwanjani hapo uliitikia aminah kwa kila hatua mpaka pale alipomaliza.

Baada ya kumaliza alisema kwa kuwa Dar es Salaam ni jiji la burudani anaruhusu Fiesta iendelee mpaka pale watu watakapokaukiwa na fedha mifukoni kauli iliyoibua shangwe kutoka kwa watu waliohudhuria katika tamasha hilo.

Kiba, Nature, Chid Benz wafunika

Katika tamasha hilo walihudhuria wasanii mbalimbali akiwamo msanii mwenye mashabiki wengi, Ali Kiba ambaye alipanda jukwaani akiwa katika mwonekano wa vazi la kifalme huku akiwa ameshika bakora ndefu.

Akiwa ameongozana na wasanii kutoka Lebo ya Kings Music, aliwakonga nyoyo maelfu ya watu waliofurika viwanjani hapo kwa kuwaimbia nyimbo za zamani na mpya ikiwamo ya ‘kadogo’, toto, mwambie sina na masozy alizoshirikiana na wasanii wa lebo ya Kings Music.

Wasanii wengine waliopanda stejini na kuwainua watu vitini muda wote ni Juma Nature na Chid Benz ambao kupitia vibao walivyowahi kutesa navyo vilisababisha watu wasitake washuke jukwaani. Wasanii wengine waliokuwepo ni Vannesa Mdee, Chegge, Dogo Janja, Sogy Doggy, Bilnas, Mafik, Julie, Rich Mavoko, Fid Q na Kristian Bella.