Mbege ilivyofanikisha safari ya muziki ya Benson Hauzimi

Saturday July 21 2018

 

By Nasra Abdallah, Mwananchi [email protected]

Mapenzi ya upepo,

Maana bendera mama we,

Mwenzako moto hauzimi, hauzimi,

Mwenzako moto hauzimi.

Basi slow temple,

Namaliza sabuni,

Mwenzako moto hauzimi, hauzimi,

Mwenzako moto hauzimi.

Hayo ni baadhi ya mashairi ya wimbo wa “Hauzimi” wa Benson Willium, unaofanya vizuri kwa sasa katika chati mbalimbali za muziki nchini.

Moja ya vivutio vikubwa katika wimbo huo mbali na ujumbe wa kubembeleza katika mapenzi, ala zinazoambatana na mashairi hayo ni balaa.

Mwaka 2011 Benson alitoka mkoani Arusha kuja jijini dar es Salaam kutafuta studio nzuri ya kurekodi nyimbo zake, kwa mujibu wa mahojiano na Mwananchi.

Hata hivyo, anasema katika harakati zake hizo wimbo wake alioutengeneza na kuusambaza kwenye redio mbalimbali, haukutoka kwa kile alichoelezwa kuwa haukukidhi viwango.

Hivyo akarudi Arusha kujipanga upya, ikiwa ni pamoja na kutafuta fedha za kuingia tena studio kutengeneza wimbo bora zaidi unaoweza kukubalika. Alisaka fedha hizo kwa kutumbuiza katika kumbi mbalimbali za harusi.

Lakini fedha alizokuwa akipata hazikumtosha kudunduliza kwa kuwa alihitaji kuvaa, kula na mambo mengine muhimu. Baada ya kuona imekuwa vigumu kukamilisha ndoto, alikwenda kuchimba madini, lakini nayo ilikuwa ni kazi ngumu kwake.

Wakati akiwa anawaza nini cha kufanya, alikuwa akisikia matangazo kuhusu shoo mbalimbali zilizokuwa zikifanyika viwanja vya Escape One.

“Moja ya mambo niliyosikia ni tangazo la Fiesta la Kikwetukwetu,” anasema Benson. “Nilipanga kwenda kuuza mbege (pombe inayotengenezwa kwa ndizi na ulezi na maarufu mikoa ya kaskazini.”

Japokuwa wazo lake lilikuwa limechelewa, meneja alimruhusu kuuza kinywaji hicho, kazi aliyoifanya kwa miezi sita na baadaye uongozi wa eneo hilo ukamuweka upande wa vinywaji vikali.

Wakati akiendelea kuhudumu katika ukumbi huo, alibahatika kuingia bendi ya Skylight baada ya kumuona kiongozi wao aliyemtaja kwa jina la Jenico ambaye anasema alishangazwa na kipaji chake. Benson alikuwa akiimba huku akifanya kazi ya kuhudumia wateja.

Harakati za Benson hazikuishia hapo, kwani mwaka 2016 usiku wa kuvunja kamati ya Fiesta, aliomba tena nafasi ya kuonyesha kipaji chake cha kuimba katika onyesho la B Band ya Banana Zoro.

“Siku hiyo kulikuwa na wageni mbalimbali, (mbunge wa Mtama) Nape Nnauye ambaye wakati huo alikuwa Waziri wa Habari, (mkururugenzi wa vipindi wa Clouds), Ruge Mutahaba na wageni wengine,” anasema.

Japokuwa anasema awali ilikuwa vigumu kuaminiwa kama anaweza, lakini mshsreheshaji wa siku hiyo, Mussa Hussein ambaye ni mtangazaji wa Clouds Media, alimruhusu.

“Nilihakikisha napambana na kumuomba bosi wangu awaambie waniruhusu nipande jukwaani kuimba, ndipo nilipopewa nafasi na kuimba wimbo wa John Ligend, mwanamuziki ambaye ni mmoja wa watu walionivutia kuingia kwenye muziki.

“Ninashukuru baada ya kumaliza Banana alinipa ofa ya kufanya kazi na bendi yake, Ruge naye aliniita ofisini kwake kesho yake na kunitaka nijunge katika Jumba la Kukuza Vipaji (THT), ambalo yeye ni kiongozi wake na pia Nape aliahidi kunisaidia pia,” anasema.

Hata hivyo anasema aliamua kwenda THT, kwani aliamini kuna msaada zaidi ikiwemo kuwezeshwa kujifunza kutumia vyombo na kupata elimu zaidi ya muziki, jambo ambalo limemsadia kumtoa kimuziki hadi leo anajulikana na kujikuta mashabiki wakimpa jina la Benson Hauzimi.

Ngoma ya Hauzimi

Anasema ngoma yake ya Hauzimi ni wazo alilokuwa nalo, ila akampatia Jay Melody kufanya kazi ya utunzi.

Benson anasema wimbo huo unaelezea namna gani mtu anavyompenda mpenzi wake na mambo ambayo anamfanyia anayoona kabisa kuwa hataki tena kuwa naye huku akiwa hajui hasa nini kosa.

Pia anasema yanayozungumzwa katika wimbo huo baadhi ya mambo yalishawahi kumtokea na ndio maana hata akauimba kwa hisia.

Hata hivyo anasema tangu aachie wimbo huo, baadhi ya wasanii wakubwa ambao hakuwategemea wamempigia simu kutaka kufanya naye kazi akiwemo Izzo Business ambaye tayari wameshatengeneza naye remix ya wimbo wake wa ‘remote’, unaotarajiwa kutoka hivi karibuni.

Pia Dogo Janja ni kati ya watu waliokubali wimbo wake huo hadi kufikia hatua ya kujirekodi akiwa anauimba na kuutupia kwenye mitandao ya kijamii.

Vilevile anasema anashukuru kuungwa mkono na kupata ‘sapoti’ kutoka kwa wasanii wa Arusha wakiwemo akina Joh Makin, G-Nako na wengineo.

Anasema kwamba matarajio yake kwa sasa ni kuendelea kufanya vizuri, kwani Hauzimi ni kionjo tu, huku akidai zinazokuja zitakuwa bab’ kubwa zaidi.


Advertisement