Meneja hoteli aanika mchongo wa Ebitoke ulivyopangwa kumvamia Mlela

Muktasari:

Meneja wa hoteli ya Protea aanika mpango ulivyosukwa wa Ebitoke kumfanyia vurugu Mlela kwenye mkutano wake na waandishi wa habari.

Dar es Salaam. Saa chache baada ya kutokea vurugu katika mkutano wa msanii wa filamu nchini Tanzania, Yusufu Mlela na waandishi wa habari, meneja wa hoteli aanika kila kitu.

Vurugu hizo zilitokea leo Jumatatu  Novemba 11,2019 katika hoteli ya Protea Dar es Salaam ambapo msanii wa vichekesho, Annastazia Exavery maarufu Ebitoke kuvamia mkutano wa waandishi wa habari na Mlela na kuanza kumpiga mpenzi wake wa sasa.

Pamoja na waandishi kutoamini kama kilichotokea kilikuwa na ukweli au ni kick, Mlela alisisitiza kuwa hakukuwa na mpango wowote uliofanywa kuhusu hilo na kusikitikia kitendo kilichofanywa  na Ebitoke ambaye aliwahi kuwa mpenzi wake.

Mwananchi haikuridhika na majibu hayo na kumtafuta meneja wa hotel, aliyejitambulisha kwa jina la Suleiman Victor ambaye  alianika mpango wote ulivyosukwa wa kufanywa kwa tukio hilo.

Victor amesema ilikuwa jana Jumapili ambapo Mlela alienda kuweka 'booking' ya kufanya mkutano na waandishi leo na kati ya mambo aliyoambiwa na msanii huyo ni kwamba kuna mchezo wataufanya.

"Alikuja hapa hotelini na kutaka sehemu ya kufanya mkutano kwa leo lakini kati ya vitu alivyoniambia ni kwamba kuna drama wataifanya katika mkutano huo japokuwa hakuniweka wazi ni nini wangefanya.”

"Pia kama ningejua drama yenyewe ndio hii nisingekubali kwa kuwa eneo letu hilo tunapokea wageni mbalimbali na kama mnavyoona ukumbi wa mkutano upo jirani na eneo la mapokezi hivyo isingeleta picha nzuri kwa hoteli lakini ndio hivyo imeshatokea,” amesema

“Kikubwa wametulipa gharama za vitu walivyoharibu na tunachoshukuru leo hakukuwa na wageni wengi,"amesema.

Aelezea Ebitoke alivyotinga hotelini hapo

Victor amesema Ebitoke alifika mapema na gari ambalo lilimuondoa eneo hilo na hawakupishana na kuwasili kwa kina Mlela.

Hata hivyo, baada ya kina Mlela kushuka na kuingia kwenye mkutano Ebitoke yeye alibaki kwenye gari hilo na dereva ambaye ni mwalimu wao wa mazoezi yeye na Mlela anayeitwa Denzel Condrad.

"Mkutano ukiwa unaendelea ndani, kaka mmoja aliyevaa kaptura nyeusi  ambaye ndiye alikuwa akiratibu mkutano akaenda kumchukua Ebitoke.

"Ghafla tukaona watu wanapigana huko ndani ya ukumbi na sisi kuja ili wasituharibie mali zetu lakini baadaye Mlela tulizungumza na akanitaarifu kuwa ndio drama aliyenieleza jana hapo naye hakutegemea kama ingekuwa hivyo," amebainisha Meneja huyo.

Aliyepigwa atoa neno

Kwa upande wake msichana aliyepigwa Princess Ester, amesema Ebitoke amemuumiza kwenye ziwa na kueleza alichomfanyia sio sawa kwani yeye hana kosa lolote.

"Ebitoke angepaswa kugombana na mwanaume wake na sio mimi, pia akubali kuwa ameachwa kwa nini anamganda mtu ambaye yupo kwenye mahusiano mengine na isitoshe mimi na Mlela tuna mwaka sasa tangu tuwe wapenzi.”

"Hizo drama walizokuwa wanaonyesha kwenye mitandao mie nilijua ni mambo ya kazi lakini kumbe mwisho wa siku wakawa wapenzi kweli,” amesema

"Kitendo alichonifanyia sikubali kiishe hivihivi kwani amenijeruhi na kunidhalilisha," amesema msichana huyo anayejulikana kwa jina la Beyonce huku mwenyewe akijitambulisha kuwa jina lake halisi ni Princess Ester.