Meneja wa Ali Kiba aeleza kilichowashinda kudhamini Wasafi Festival

Wednesday January 2 2019

 

By Nasra Abdallah, Mwananchi

Uongozi wa msanii Ali Kiba, umeeleza sababu za kukwama kudhamini tamasha la Wasafi ambalo lilianza kutimua vumbi Novemba 24 mwaka jana.

Novemba 5, mwaka jana wakati Diamond akitangaza rasmi kuanza kwa tamasha hilo, alisema angefurahi kama hasimu wake Ali Kiba naye angeshiriki.

Baadaye Ali Kiba kupitia ukurasa wake katika mtandao wa Instagram, alishukuru kwa mwaliko huo na kusema kutokana na ratiba yake kumbana atakachofanya ni kuwa mmoja wa wadhamini wa tamasha hilo kupitia kinywaji chake cha Mofaya.

Kutokana na majibu hayo Diamond alimuomba meneja wake Salam Sharif azungumze na uongozi wa Kiba kuona namna gani wataweza kulidhamini tamasha hilo.

Tayari tamasha hilo limeshafanyika katika mikoa sita mpaka sasa ikiwamo Mtwara, Iringa, Morogoro, Sumbawanga (Rukwa), Mwanza na Tanzania Zanzibar bila udhamini huo.

Akizungumza na Mwananchi, Meneja wa Ali Kiba, Christina Mosha ‘Seven’ alisema hawakudhamini tamasha hilo baada ya kushindwa kufikia makubaliano.

Alisema: “Labda wasubiri mwaka huu kama wataendelea na tamasha lao tunaweza kuwadhamini.”

Katika hatua nyingine Seven alisema mwaka huu Ali Kiba anatarajiwa kufanya shoo kwenye mikoa mbalimbali.

“Tulieni ratiba ya hizo shoo mikoani tutaiweka hadharani hivi karibuni, ” alisema.

Advertisement