Miss Rwanda apewa gari, mshahara wa kila mwezi

Muktasari:

Rwanda imempata mrembo atakayeiwakilisha nchi hiyo katika Miss World, shindano litakalofanyika nchini Thailand, Desemba mwaka huu.

Rwanda. Safari ya kuelekea kushiriki Miss World 2020 imekamilika Rwanda baada ya kumpata mwakilishi wao, Naomie Nishimwe aliyetwaa taji la Miss Rwanda.

Kwa ushindi huo, Naomie amepewa zawadi ya gari na atalipwa mshahara wa kila mwezi.

Naomie alitwaa taji la Miss Rwanda, katika fainali zilizofanyika mwishoni mwa wiki kwenye ukumbi wa mikutano wa Intare Arena nchini humo.

Mrembo huyo ambaye alishiriki katika Miss Kigali, alichuana na warembo wengine 19 ambapo mbali ya kuwa Miss Rwanda pia alishinda kipengele cha Miss Photogenic.

Naomie ataiwakilisha Rwanda katika Miss World, shindano linalotarajiwa kufanyika Desemba mwaka huu nchini Thailand.

Kutokana na ushindi huo Naomie alipata zawadi mbalimbali ikiwemo gari aina ya Suzuki Swift lenye thamani ya Sh43 milioni.

Pia shirika linalojishughulisha na masuala ya chakula Afrika la Africa Improved Foods (AIF), lilijitolea kumlipa mshahara wa Sh1.9 milioni kila  mwezi.

Katika kinyanganyiro hicho mrembo, Umwiza Phionah alishika nafasi ya pili na wa tatu alikuwa Umutesi Denise ambao wote waliondoka na Sh3 milioni kila mmoja.

Warembo wengine waliong’ara katika shindano hilo ni Ndenga Teta alitwaa taji la Miss Urithi, wakati Alliance Irasubiza aliibuka kidedea kwa kuwa mrembo maarufu.