Miss Tanzania aendelea kung’ara China

Pamoja na kura kumwangusha katika mashindano ya Head to Head, mwakilishi wa Tanzania katika mashindano ya Miss World, Queen Elizabeth Makune ameendelea kung’ara katika shughuli mbalimbali za fainali hizo zinazoendelea Sanya, China.

Elizabeth ambaye Desemba 8, atapanda katika jukwaa la Miss World nchini humo, ni miongoni mwa washiriki wanaotajika kufanya vizuri mpaka sasa.

Ingawa kura zimemwangusha katika mashindano ya Head to Head yaliyofanyika mwishoni mwa wiki, binti huyo aliyetwaa taji la Miss Tanzania akitokea Kanda ya Dar es Salaam ameendelea kung’ara kutokana na kujiamini kwake.

Mapema wiki hii video ya mlimbwende huyo kutoka Kinondoni ilienea mtandaoni ikimwonyesha akizungumza kwa kujiamini alisema huenda akawa mrembo wa kwanza kutoka Tanzania kutwaa taji la Miss World.

Alisema jukwaa la Miss World linampa nafasi ya kujitambua na kujipambanua kama mwanamke mwenye ndoto ya kubadilisha maisha.

Mahojiano hayo yalionyesha kuwakuna watu wengi mitandaoni na kumshangilia kwamba hata asiposhinda huo ni ushindi tosha.

Mwanamuziki Ben Pol aliandika kwa utani akisema: “Mimi nilikuwa fan (shabiki) wako kitambo lakini sasa nimepitiliza nimekuwa air condition (kiyoyozi).

Muandaaji wa mashindano hayo nchini Basilla Mwanukuzi amesisitiza Watanzania kuendelea kumpigia kura mrembo huyo ili kumuweka katika nafasi nzuri ya mashindano hayo.

Amesema: “ Watanzania tufanye jambo moja muhimu la ku download application ya Mobstar Ili tuweze kumpigia kura mrembo anayetuwakilisha kadri tuwezavyo. Tukimpigia kura Queen Elizabeth Makune maana yake tumeipigia kura Tanzania.”