Msanii Rosaree afungiwa miezi sita, atozwa faini ya Sh2 milioni

Muktasari:

Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) limemfungia msanii wa Bongo Fleva, Rozaree Robert maarufu Rozaree kujihusisha na sanaa kwa muda wa miezi sita pamoja na kumtoza faini ya Sh2 milioni.

Dar es Salaam. Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) limemfungia msanii wa Bongo Fleva, Rozaree Robert maarufu Rozaree kujihusisha na sanaa kwa muda wa miezi sita pamoja na kumtoza faini ya Sh2 milioni.

Basata imechukua uamuzi huo kwa madai kuwa wimbo wa Vitamin U ambao msanii huyo ameshirikishwa na wasanii wa Kenya umekiuka maadili.

Akizungumza na Mwananchi leo Alhamisi Novemba 14, 2019 kaimu katibu mtendaji wa Basata, Onesmo Kayanda  amesema kati ya Sh2 milioni anazotakiwa kulipa, Sh1 milioni ni kwa ajili ya kosa la kukiuka maadili na Sh1 milioni kwa kosa la kwenda kufanya kazi hiyo  Kenya bila kibali cha Basata.

"Kilichoonyeshwa kwenye video ya Vitamin U na msanii wetu Rozaree hakikubaliki katika maadili ya Mtanzania hivyo tulimuita Novemba 6, 2019 na kumsomea makosa yake.”

“Kamati ya maadili ilifikia uamuzi wa kumfungia miezi sita kutojishughulisha na sanaa na kumtoza Sh2 milioni ya faini kwa makosa mawili aliyoyafanya," amesema Kayanda.

Amesema pamoja na hatua hiyo Rozaree ana nafasi ya kukata rufaa ndani ya siku 30 kama hajaridhika na adhabu hiyo, rufaa ambayo ipo ngazi ya Waziri mwenye dhamana na sanaa.