Mtoto wa Banza Stone afunguka alivyopata tabu kutoboa kimuziki

Monday January 7 2019

 

By Nasra Abdallah, Mwananchi [email protected]

Licha ya baba yake kuwa maarufu kwa kufanya kazi katika bendi kubwa hapa nchini, mtoto wa pekee wa marehemu Banza Stone, Hassan Ramadhani Masanja ‘Hanstone’, amesema kutoboa kwenye muziki si kazi rahisi kama watu wanavyofikiria.

Akihojiwa na gazeti la Mwananchi, Hanstone (pichani) ambaye amepata umaarufu kupitia kibao cha Iokote alichoshirikishwa na Maua Sama, alisema kutoka kwa msanii hakutokani na umaarufu wa mzazi bali ni nguvu ya msanii mwenyewe.

Akijitolea mfano alisema ameanza kusota kimuziki tangu akiwa shule ya msingi wakati huo baba yake akiwa katika tasnia ya muziki, lakini amekuja kutoboa mwaka jana.

Akielezea vitu ambavyo amekuwa akivikumbuka kwa baba yake, msanii huyo mwenye miaka 19 kwa sasa, alisema alikuwa akimsihi asome ndipo aingie kwenye muziki, lakini kwa bahati mbaya wakati akimaliza elimu ya msingi baba yake alianza kuugua mpaka pale umauti ulipomkuta.

Aliongeza kuwa licha ya kufanya muziki tofauti, lakini baba yake, alikuwa msaada katika kumrekebishia mashairi ya nyimbo zake za bongo fleva ambapo anaeleza mpaka sasa anazo nyingi amezihifadhi na ataziachia muda utakapofika.

“Kama mnavyojua baba yangu alikuwa mtunzi mzuri wa mashairi japokuwa mimi sikuwa nafuatilia sana muziki wa bendi, hivyo nami nilikuwa nikiandika mashairi yangu nampelekea akanirekebishie, kwa kweli nitamkumbuka daima,” alisema.

Alisema katika kumuenzi baba yake ana mpango wa kuvirudia vibao vyake ambavyo amewahi kuimba na kuviweka katika wimbo mmoja kazi ambayo ameeleza mashabiki wa Banza na yeye wategemee kuisikia ndani ya mwaka huu.

Enzi za uhai wake Banza aliyefariki Julai 2015, aliwahi kutamba na vibao kama Mtu Pesa, Mtaji wa Masikini, Elimu ya Mjinga, Supu ya Kuku wa kienyeji na Nilivyoanza Masanja.

Kuhusu wimbo wa Iokote, Hanstone alisema anashukuru imeweza kubadili maisha yake ikiwemo kufanya shoo katika mikoa mbalimbali na kuweza kuanza kujitegemea mwenyewe kimaisha.

“Namshukuru sana Maua kwa kunichagua niimbe nae wimbo huo wa Iokote ambao awali alitakiwa kuimba na msanii mkubwa lakini akaniona mimi ninaweza. Naahidi sitamwangusha,” alisema msanii huyo.

Advertisement