Mzee Yusuf apata kigugumizi kufafanua ‘Narudi Mjini’

Muktasari:

Tangu ameposti Narudi mjini, Alhaji Mzee Yusuf katika kurasa yake ya mtandao wa kijamii, amekuwa akiweka picha za wadau wa muziki wa taarabu na waimbaji baadhi wa muziki huo

Dar es Salaam. Alhaji Mzee Yusuf amesema watu waendelee kutabiri wanachotabiri juu ya maneno yake ‘Narudi mjini’ aliyoandika Machi 12, 2020 katika ukurasa wake wa mtandao Instagram.

Kauli hiyo ya ‘Narudi Mjini’ ya Mzee Yusuf imewaibua wadau mbalimbali wa muziki na wapenzi wake kila moja akisema lake kuhusu suala hilo.

Akizungumza na www.mwanaspoti.co.tz, Mzee Yusuf amesema tangu alipopost kauli hiyo amepata simu nyingi za watu kutaka ufafanuzi juu ya andiko hilo.

Amesema wapo watu wanaomwambia sehemu ya kufanyia Tamasha na kuchaguliwa wadhamini wakiwa na utabiri kuwa anarudi mjini kuimba.

"Yaani sikutegemea mapokezi makubwa ya andiko langu la ‘narudi mjini’ kupokelewa na watu wengi hivi, yaani hadi nimeshangaa, na ningeshangaa zaidi wewe usinipigie simu kuniuliza hili sababu tulikuwa tunakesha wote pindi naimba taarabu hahahaha.”

“Wacha watu waendelee kutabiri, jambo hilo wanalodhani la kurudi mjini katika taarabu likifika basi kila mtu atajua," amesema Alhaji Mzee Yusuf.

Tangu ameposti Narudi mjini, Alhaji Mzee Yusuf katika kurasa yake ya mtandao wa kijamii, amekuwa akiweka picha za wadau wa muziki wa taarabu na waimbaji baadhi wa muziki huo huku aliandika maneno haya "Narudi mjini" ndugu zangu mnipokee, hapa nawaza nitaimba na wasanii wale wale au nichague wengine, maana wapo waliokuwa tayari wameshaanzisha bendi zao.

Miongoni mwa waimbaji 'aliowaposti' ni Haji Boha aliwahi kuwa kiongozi wa bendi yake ya Jahazi, Prince Amigo, mtoto pori walikuwa waimbaji wa bendi ya Jahazi ya Mzee Yusuf, pamoja na Saidi Mdoe mdau mkubwa wa muziki wa taarabu.

Alhaji Mzee Yusuf mwaka 2016 alitangaza kuachana na muziki na kuingia katika masuala ya kufundisha dini na kutoa dawa kabla ya kwenda kuhiji Makka na jina lake hapo ndipo lilipobadilika na kuanza kuitwa Alhaji

Mzee Yusuf baada ya kutangaza kuachana na muziki, watu wengi walikuwa wanamuomba arudi katika muziki kutokana na muziki wa taarabu kuyumba, lakini Mzee Yusuf aliendelea kushikilia msimamo wake kuwa muziki huo ni kinyume na maadili ya Dini ya Kiislam.