Nandy aanza safari ya kuanzisha ‘THT’ yake

Muktasari:

  • Msanii wa Bongo  Fleva nchini Tanzania Faustina Charles maarufu Nandy yupo mbioni kuanzisha kituo chake cha kuendeleza vipaji vya wasanii wa muziki huo huku akitaka wapitie njia alizopita yeye kufundishwa muziki huo.

Dar es Salaam. Unakumbuka Nyumba ya kukuza Vipaji’ Tanzania House of Talent (THT), ilivyozalisha wasanii wengi wanaofanya vizuri kwenye soko la muziki.

Wasanii hao ni pamoja na Amini, Nandy, Ben Pol,Barnaba, Linah, Mwasiti na wengineo.

Ni kutokana na matunda hayo, msanii wa Bongo Flea nchini Tanzania, Nandy naye yupo mbioni kuanzisha THT yake ili kuzalisha wasanii wengine ambao watapitia njia za mafundisho wa  muziki walizopita wao.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatatu Januari 20,2020, Nandy amesema alipofikia naye ana kila sababu ya kuwashika wengine mkono wenye vipaji vya kuimba.

Katika kulitekeleza hilo, msanii huyo anayetesa na wimbo wa Kiza Kinene amesema tayari ameshaanza kununua baadhi ya vifaa.

“Nimeshaanza kukusanya vifaa vya muziki ambapo huwa katika kila shoo ninayopata nanunua kimoja  kimoja nia ikiwa wasanii nitakaokuja kuwasimamia wapitie njia tulizopitia sisi kufundishwa muziki ikiwamo kutumia vyombo,” amesema.

Wakati kuhusu suala la studio Nandy amesema tayari anayo na hata wimbo wa ‘Kiza kinene’ aliowashirikisha wasanii Saut Soul kutoka nchini Kenya wameirekodia hapo.

Kama vile haitoshi hata wimbo wa ‘Kata’ alioshirikishwa kuimba na msanii wa Bongo Fleva, Ommy Dimpoz wameutengenezea hapo.