Ndani ya boksi: King Kiba una deni na mashabiki usijikaushe

Sunday March 15 2020

 

By Dk Levy

King Kiba. Yule Ally Saleh wa Kariakoo ana sauti ya pekee yenye upekee. Huhitaji kupata ngoma yake mpya ili umuelewe. Na inawezekana ngoma mpya isikupe ile kitu yenyewe toka ndani. Kama ambavyo ukisikia ngoma zake kadhaa za nyuma. Ukimsikia kwenye moja tu kati ya zile za zamani utakuwa shabiki wake namba moja.

Amini nakuambia.

Elizabeth Michael muite ‘Lulu’. Aliwahi kubanwa na wadaku wa mjini. Juu ya ukaribu wake na Ali. Of coz akili za wadaku ilikuwa kutaka kujua ‘wanashea’ nini katika jiji hili. Lulu na ile sura isiyo na majibu ya kama amependa au kakerwa na swali. Alitoa jibu kwa utulivu sana kwamba wao ni marafiki wa kawaida na hakuna la zaidi kati yao.

Akaenda mbali zaidi. Akikiri wazi kabisa kuwa yeye ni shabiki wa King Kiba. Na anachovutiwa nacho toka kwa bishoo huyo wa Kariakoo ni sauti. Alisema haya miaka mingi iliyopita.. Maisha ya usiri ya Kiba yalifanya watu waishie kuhisihisi tu. Dunia ya leo na wadaku hawajawahi kuvutiwa na aina ya maisha ya Kiba.

Elizabeth Michael unamfahamu vyema? Mmoja wa warembo wenye tani nyingi sana za mvuto mjini. Kila kidume mjini kikitamani kuwa karibu naye. Lakini kumbe naye anakwama mno kwenye sauti ya bishoo wa K’koo. Lulu aliikiri kuchanganyikiwa na ile sauti ya Kiba. Naye ni miongoni mwa mashabiki wa Kiba. Kama unaweza kumteka Lulu, unataka nini zaidi? Kama Lulu na pozi zake alikiri hivyo. Unadhani ni madem wangapi mjini wanavurugwa na King Kiba? Kuna kundi kubwa la totoz na mabishoo wanaozimika na kazi za Kiba hapa mjini. Hilo liko wazi. Ni mmoja wa wanamuziki ambaye amedumu kisanaa huku upepo wa muziki ukimfuata yeye popote aendapo. Wengi alioanza nao wamekwama.

Si kwa sauti tu. Ingawa sauti imekuwa silaha yake kubwa ambayo hata staa wa dunia Robert Kelly ‘R Kelly’ alishangazwa nayo. Wameshafanya ngoma pamoja akiwemo Chameleone wa Uganda. Achana na Cinderela hapo gari lilikuwa halijapata moto sana. Ingawa ilikuwa hits song ya kibabe sana.

Advertisement

Unyama wa Kiba unaupata kwenye ‘Nakshi Nakshi’ na ‘Maki Muga’. Kuna ‘Karim’, Hadithi na ‘Mapenzi yana run dunia’. Kutana na ‘Single Boy’, ‘Dushelele’ na nyinginezo ambazo ujazo wake huupati kwa hawa masela wa sasa. Ndo maana unaona anahama na watu.

Pamoja na yote hayo. Unafahamu kwa nini Kiba hana makeke kama wengine wa kizazi chake? Hili swali watu wengi sana wanajiuliza. Kuna sehemu anauza mechi na kuwachomesha sana mahindi mashabiki wake. Kiba anashindwa kusoma nyakati. Pamoja na ubora wake huo lakini kusoma mchezo na nyakati hapo anakwama. Yes.

Pamoja na sauti yake ya pekee. Utunzi wenye akili utulivu na pia uwepo wa mashabiki kibao wa kike na wa kiume. Huku mastaa kibao wenye ‘bezi’ kubwa ya mashabiki kama Lulu wakiweka wazi kabisa kumuelewa mchizi huyo wa Kariakoo.

Lakini bado amekuwa nyuma ya mstari wa mastaa wa muziki wa leo. Hili liko wazi achana na kelele za mashabiki. Kinachomtokea kiliwakuta wengi. Wanafanya kitu bora kwenye sanaa. Lakini mafanikio yao na kukaa midomoni mwa watu katu hayaakisi ule ubora wao. Kuna wale wepesi lakini wanakimbiza zaidi.

Hii ipo dunia nzima. Mwenye kipaji kikubwa anakosa mafanikio yenye ukubwa sawa na wale wenye vipaji vyepesi.

Katika akili ya kawaida isiyo na mawaa ya pombe hakuna ubishi kuwa King Kiba ana uwezo wa kufanya zaidi ya alichowahi kukifanya katika muziki.

Namaanisha Tanzania na Afrika kwa ujumla kuna kitu inasubiri kukisikia ama kukiona kikifanywa na King Kiba katika tasnia ya burudani.

Hata uwe na mashabiki wenye majina na wafuasi wengi kiasi gani, kama hakuna unachofanya kukata kiu iliyowasukuma kukufuata utabaki kuelezea historia ulivyofanya vizuri huko nyuma na si vipya vinavyokwenda na wakati uliopo.

Sawa! Ukitoa ngoma kali baada ya kukaa kimya miaka miwili mitatu wataikubali, lakini utakuwa umewasubirisha sana na pengine watapungua na kutafuta burudani mpya kutoka kwa wasanii wapya au waliopo wenye angalau kidogo.

Kuitwa msanii maana yake unafanya sanaa, sasa ukiwa mwimbaji kama King Kiba unakaa muda mrefu kabla ya kutoa wimbo, mashabiki wanakutetea, wanakujengea hoja mpaka wanashindwa.

Ninaweza kusema King Kiba anadaiwa na mashabiki wake, kuna wanachotaka kukisikia kutoka kwake mara kwa mara, aache kujikausha, ukimya siyo mpango katika dunia inayohitaji burudani kupunguza stresi za maisha.

Advertisement