Ndoa hizi zinabamba kinoma

Friday February 22 2019

 

By Rhobi Chacha

KWA sasa ishu inayombana huko mtaani na kwenye mitandao ya kijamii ni ndoa ya aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa katika Serikali ya Awamu ya Nne, Profesa Juma Kapuya.

Profesa Kapuya, ambaye amewahi pia kuongoza wizara nyingine kwenye utawala wa Rais Jakaya Kikwete, amefunga ndoa na mkewe Mwajuma Mwiniko mwishoni mwa wiki iliyopita.

Hata hivyo, ndoa hiyo imeonekana kuwa gumzo kwelikweli hasa kwenye mitandao ya kijamii kutokana na kile kinachodaiwa wawili hao kupishana umri kwa mbali.

Kwa sasa Profesa Kapuya, ambaye pia aliwahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Urambo kabla ya kudondoshwa na Magdalena Sakaya, ana miaka wa miaka 74.

Hapa Mwanaspoti linakuletea ndoa nyingine ambazo zimebamba kinoma kwenye jamii kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo umaarufu mkubwa wa wahusika.

Benny Kinyaiya

Kabla hata ya ndoa ya Profesa Kapuya, picha zikimuonyesha Ben Kinyaiya akifunga ndoa na mwanamke aliyedaiwa kuwa mchumba wake wa siku nyingi, zilianza kutikisa kwenye mitandao ya kijamii.

Picha hizo zikafuatiwa na video fupifupi zikimuonyesha Ben na mkewe huyo wakiwa kwenye sherehe wakisakata rhumba na wageni wengine ndani ya ukumbi.

Kama kawaida huko kwenye mitandao watu hawakulala kila mmoja akizungumza lake kuhusiana na ndoa hiyo, ambayo imeacha gumzo kwelikweli.

Picha zilimuonyesha Ben akiwa kwenye ofisi ya Serikali huku ikielezwa kuwa ni ya Mkuu wa Wilaya mmoja hapa jijini Dar es Salaam, ambapo wawili hao walikuwa wakila kiapo cha ndoa.

Mengi yamesemwa na yanaendelea kusemwa kuhusiana na ndoa hiyo, lakini Ben mwenyewe ameibuka na kuwapasha wanafuatilia ndoa yake kuacha.

Juzi Ben alikuwa akihojiwa na EFM Radio ambapo, aliwapasha wambeya wanaofuatilia ishu zake kuacha mara moja kwa kuwa, hayawahusu.

“Ngoja leo niwafungukie hawa watu vizabizabina kwenye mitandao ya kijamii kwani, kazi yao wakiamka hata mswaki hawapigi wanaongea habari za watu kama wana uhakika nazo.

“Sasa naawambia hata kama mfano nimeoa mambo yangu hawayahusu. Mnajifanya kumjua sana yule mwanamke kama wao ndio mama mzazi wao,” alisema Ben.

Reginald Mengi na Jacqueline Ntuyabaliwe

Bilionea wa ukweli nchini na mtu wa watu, Reginald Mengi naye ndoa yake na Miss Tanzania 2000, Jacqueline Ntuyabaliwe. Wanandoa hawa ni miongoni mwa watu maaarufu zaidi nchini kutokana na kushiriki kwenye kazi za kijamii huku wakimiliki makampuni makubwa ambayo, yamewezesha vijana wengi kupata ajira.

Mengi na Jacqueline walifunga ndoa kwenye Visiwa vya Shelisheli mwaka 2015 na kwa sasa wana watoto wawili mapacha.

Mama Diamond na Shamte

Haikuwa ikivuma sana hadi ilipowekwa bayana na mhusika mwenyewe. Ndoa hii ilifungwa kimyakimya kati ya Sandra na Shamte Maisala.

Ndoa ya Sandra, ambaye ni mama wa staa wa Bongo Flava, Diamond Platinumz, ilifungwa mwishoni mwa mwaka 2017 na sasa imekuwa ikibamba kinoma kutokana na aina ya maisha ya wawili hawa kuvutia wengi.

Sandra aliwahi kukaririwa akiwapasha watu wanaoshobokea ndoa yake kuacha kwani, umri unawaruhusu na ndio sababu wamefunga ndoa.

Uwoya na Dogo Janja

Ndoa ya Malkia wa Bongo Movie, Irene Uwoya ni msanii wa Bongo Flava, Dogo Janja, nayo imesumbua kinoma miongoni mwa ndoa za mastaa wa Bongo.

Huko kwenye mitandao mengi yamezungumzwa kuhusiana na ndoa hii, lakini kamwe hayakuzuia kitu kwani, watu walifurahi siku ya tukio na ubwabwa ukaliwa vilevile.

Hata hivyo, wengi hawakuwa wakiamini kama kweli kuna ukweli ndani ya ndoa hii na baadhi walidhani ni maigizo, lakini walisubiri kuona filamu mpaka sasa giza tu. Hapa ikabainika ni kweli wawili hawa wamefunga ndoa na walikuwa wakionekana maeneo mbalimbali ya bata wakiwa pamoja. Lakini kila chenye mwanzo kina mwisho, kwa sasa ndoa ya Uwoya na Janja imebaki kuwa historia na kila mmoja amekiri kuwa ndoa yao imesambaratika na kila mmoja ameshika hamsini zake.

Riyama na Mystrerio

Kama wewe ni mpenzi wa Bongo Movie, basi ushakutana na vichambo na maneno ya shombo kali ya Riyama. Sasa bana pamoja na vichambo vyake vyoteee huyu dada kwa Rapa Mysterio anatulizana kimya.

Ndio wawili hawa walibamba sana wakati wakifunga ndoa yao Juni 2016 na licha ya maneno mengi ya waja huko kwenye mitandao, lakini wenyewe wapii hawasikilizi lolote wanasonga mbele.

Kapuya na Mwajuma

Vijana wa mjini kwa sasa wanahamasishana kutafuta pesa kwa nguvu ili kuwadhibiti wazee wasiwachukulie wadada wazuri.

Kila kona kwa sasa vijana wamekuwa wakiwahoji wadada warembo, wamekosea wapi hadi wanakwenda kuolewa na wazee na kuwaacha. Lakini kauli hizo kamwe hazina mashiko kwa Profesa Kapuya, ambaye amekiri kufunga ndoa na Mwajuma na kuwa hakuna mahali alipokosea wala kukiuka maandiko matakatifu.

Profesa Kapuya amelieleza Mwanaspoti Mwajuma ni mkewe wa pili na ndio atakuwa wa mwisho kwa kuwa, hatarajii kufunga ndoa tena. Pia, amesema wanatarajia kupata watoto na mkewe huyo na moja ya sifa anazozipenda kwake ni pamoja na kujua kupika mahanjumati hasa maharage.

“Nawashangaa watu wanaohoji mimi kuoa, hivi umri unahusiana na nini kwenye mapenzi. Ukiangalia huyu mwanamke sijamtorosha shule, wala sijavunja mila, desturi pamoja na dini.

“Ama watu wanataka nikaoe mke anayefanana na bibi yangu? Jamani watu wakubali matokeo tu,” alisema Profesa Kapuya.

Advertisement