P-SQUARE: Huenda wamebadilishana vifua na wake zao hawa

Monday November 25 2019

 

By Luqman Maloto

P-SQUARE ni defunct group kwa sasa, halipo. Labda mpaka wenyewe waamue kulirejesha. Halafu kuzungumza P-Square ni kundi lililojifia ni ujima. Tuachane na hiyo stori.

Hata kuongea sababu ya pacha Paul na Peter kuvunja kundi pia ni ukale. Kipi kipya? Peter alishalalamika sana Paul alikuwa hamheshimu yeye na mkewe, Lola, na kuna wakati alimfokea mazoezini au kwenye shoo alipochelewa kidogo.

Sema nini, haitakuwa ujima kama sababu ya kundi kusambaratika itaelezwa na Paul. Maana yeye hujibu: “Ni mambo ya kifamilia na siwezi kuzungumzia familia yangu kwenye vyombo vya habari.”

Peter anasema P-Square litarudi kufanya kazi kama Paul atamheshimu yeye na Lola. Peter anasema hakuna siku alichukia kama alipoulizwa na Paul: “Kati ya mimi na mkeo nani bora?”

MAKABURI VEEPE!

Naona kama nafukua makaburi hivi? Sio shida, kwani kazikwa nani? Peter manung’uniko yake ni familia yake yote ipo upande wa Paul, ndio maana aliamua kuwekeza umakini wake wote kwa mke wake na watoto.

Advertisement

Ngoja nikun ong’oneze, ila usinione nipo nyuma sana kama hii stori unainyaka. Yule Lola ni bi mkubwa kuliko Peter. Yaani, dashboard ya Lola inasoma kilomita nyingi kuliko ya Peter. Hicho ndio chanzo.

Peter alipoanza mapenzi na Lola, watoa macho waliponda na familia ya Peter ikasema haiwezekani. Ndio hivyo, janki akawa kapenda, utamwambia nini?

Mara ndoa ikafuata, familia ikamwambia “Peter kuwa na adabu, unataka kumuoa mama yako mdogo, utapata laana!” Peter akasema awe mama mdogo, mkubwa, bibi, shangazi, kungwi na jina lingine lolote lile, yeye lazima aoe. Kwani umri si namba tu? Aliimba Aaliyah “Age Ain’t Nothing But A Number”.

Kweli mtu mzima akaoa na watoto wawili wapo kwenye akaunti yao ya uzazi. Sasa katika kumpigania mkewe, ndio akasababisha na kundi livunjike.

Gharama za kuvunjika kwa P-Square ni kubwa na hasara haielezeki. Walikuwa ndio watawala wa muziki Afrika na duniani walitembea kukusanya ngawira.

Njemba mbili zilizoishi kwenye mfuko mmoja wa uzazi miezi tisa kisha zikazaliwa siku moja, zilifanya mabalaa ambayo hakuna mwingine wa kusogelea kwa karibu Afrika. Wakafikia kiwango cha kutoza Dola 300,000 kwa shoo. Hatari sana!

YouTube P-Square wakawa ndio watawala. Video zao zikaongoza kwa kutazamwa kila walipotoa dude. Walipotengana na utawala wao ukaisha.

Peter nje ya P-Square inabidi aanze kujenga upya brand yake, kama ilivyo kwa Paul. Wakati wakiwa wawili, waliifanya P-Square kuwa brand ya muziki yenye nguvu kuliko nyingine yoyote Afrika.

Kilichopo wakati huu ni kuwa Paul ‘Rudeboy’ na Peter ‘Mr P’ wanajenga brand zao kila mmoja kwa kujitegemea. Matokeo yake Rudeboy na Mr P wanaburuzwa kwa mtaji wa hadhira mbele ya kina Davido, Wizkid hata Diamond Platnumz.

P-Square ingekuwa inafanya kazi pamoja leo, ungewakusanya Davido, Wizkid, Diamond na wengine unaowaona wakali, uwaweke kundi moja, mbele ya P-Square, wangeburuzwa.

Unajua P-Square walikuwa wameshajenga audience kubwa. Paul na Peter nje ya P-Sqaure kila mmoja inabidi aunde audience yake.

Ngoma ambazo Rudeboy anatoa, zingekuwa kwenye brand ya P-Square mbona ungekuwa mchakamchaka?

NIPO NJE YA TOPIC EEH?

Inawezekana ni uzee unanipelekesha mpaka naongea sana nje ya mada. Ni hivi, Mei 25, mwaka huu, Peter aliwaka kupitia instagram kuwa jina lake lilitumika vibaya na akatishia kumpeleka promota mahakamani.

Ni promota wa shoo iliyoitwa “7 Anivesario Pub Four”, sijui ni anivesari ya 7 ya Pub Four? Kwani mimi na Kireno wapi na wapi? Hiyo shoo ilimhusu Paul. Katika tangazo, ilitumiwa picha ya Peter na Paul pamoja na jina P-Square.

Peter akasema “wanaona bila jina langu hawawezi kupata watu!” Akaambatanisha na picha ya Paul akiwa anawasili Angola. Ndio, shoo hiyo ilifanyika Angola.

Post hiyo ya Peter ilidhihirisha ndugu mapacha wapo kwenye hatua mbaya. Sio tu hawakuwa wakiongea na Peter kuzungumza hovyo, bali hata kutakiana mabaya.

Tangu Septemba 2017, wakili wa Peter, Festus Keyamo alipowasilisha hati ya kisheria ya kutaka mteja wake (Peter) agawiwe hisa zake zote na kuvunja kundi la P-Square, ndugu wawili wameonesha hawaivi.

Tunaambiwa wanaume huwa na vifua vyenye kuhimili kuliko wanawake, kama ni hivyo, basi Paul na Peter, watakuwa wameazimana vifua na wake zao, Anita na Lola.

Kwa Paul na Peter inaonekana hayupo anayemtakia heri mwenzake (kama ambavyo Peter huiweka hadharani). Hata hivyo, wake zao hutoa picha ya tofauti.

Mke wa Paul, Anita na Lola wa Peter, hujaribu huonesha kuwa bado kuna upendo katikati yao. Na hufanya hivyo mpaka kwa watoto wao.

Novemba 18, mwaka huu, ilikuwa siku ya kumbukumbu ya kuzaliwa Peter na Paul. Kila mmoja alisherehekea mwenyewe. Paul akiwa na mastaa wenzake wa Nigeria, Peter hakuwa Nigeria.

Wao ikiwa hivyo, Lola alipost video ya watoto wake na Peter, Cameron na Alion wakiwatakia heri Peter na Paul. Alion alisema “happy birthday papa” alimuwish Peter. Cameron akasema “happy birthday uncle Paul”.

Aliona akaendelea “We love you two so much” Cameron akaongeza “We love you both” halafu Alion akamaliza “go twins”. Ukiona video unaona Cameron na Alion walifundishwa. Na nani sasa? Jibu ni Lola.

Lola pia aliweka picha ya Peter na Paul, akawatakia heri pamoja, akasema anawapenda wote. Anita pia alipost picha za Paul na Peter na kuwatakia heri pamoja, mafanikio na akaeleza anavyowapenda.

Hapo ndipo unaona Paul na Peter watakuwa wamechukua vifua vya wake zao, kama msemo wa wanaume wanavifua vyenye kuhimili kuliko wanawake unaendelea kuwepo.

Vinginevyo, Anita na Lola wanaonesha ni kiasi gani familia ni muhimu kuliko magomvi. Wanaonesha kuwa wao ni familia moja. Peter anaweza kuropoka kuhusu Paul, lakini Lola na Anita wanaendelea kulinda nafasi ya familia.

Je, post za Lola na Anita ni maigizo? Kama hawaigizi basi wanafanya vizuri. Mungu awaongoze.

Advertisement