VIDEO: Rammy Galis: Nimejifunza kitu muhimu kwa Wanigeria

Muigizaji wa filamu, Rammy Galis, amesema kufanya kazi na wasanii wa Nigeria kumemfundisha mengi ikiwamo suala la kuheshimu muda na kutojiona wa gharama kisa unamiliki gari la kifahari.

Galis (pichani) aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati wa uzinduzi wa sinema zitakazoshindanishwa kwenye tuzo za Sinema Zetu International Film Festival (SZIFF), zinazoandaliwa na kituo cha Azam Tv.

Katika uzinduzi huo uliofanyika Ukumbi wa City Mall, sinema ya Galis aliyoifanya kwa kushirikiana na wasanii kutoka Nigeria akiwamo Yvonne Jegede, Daniel Lloyd na Nicole Franklyn inayoitwa Red Flag, ndio iliyofungua dimba kuonyeshwa.

Akizungumzia utofauti wa wasanii hao wa Nigeria na wa hapa katika kufanya kazi, Galis alisema ni watu wanaojali muda na kuheshimu kazi yao bila kujali mali za thamani wanazomiliki ikiwamo magari.

“Wenzetu hawa bila kujali ana jina kubwa kiasi gani kwenye sanaa au anaendesha gari la thamani gani, unapofika muda wa kazi wao wanajali sana wanachokifanya tofauti na wa hapa nyumbani.

“Yaani nilikuwa nashangaa kila nikifika location (eneo la kuigizia), unamkuta msanii mkubwa yeye ameshawahi na gari lake la maana ameliegesha nje. Walinipa somo kwa kweli kwamba kazi inayokupa ugali wa kila siku lazima uiheshimu tofauti na hapa Bongo kisa anaendesha gari zuri msanii atataka umnyenyekee na kuja wa mwisho ili watu wote mumtazame yeye anapoingia, tubadilike,” alisema msanii huyo ambaye aliwahi kutesa na filamu ya Chausiku.

Akiizungumzia sinema hiyo ya Red Flag kuwa ya peke yake kutoka Tanzania kati ya sinema 19 zilizoingia kwenye tuzo, alisema imetokana na kutengenezwa kwa kiwango cha kimataifa.

Galis aliongeza kuwa anaamini itamfungulia njia nyingi za kuendelea kufanya kazi na wasanii wa kimataifa ndoto ambayo amekuwa nayo kwa siku nyingi.

Sinema hizo zilizoanza kuonyeshwa Februari 11, zitaonyeshwa kila siku hadi ifikapo Februari 10 mwaka huu.

Katika tuzo hizo mwaka huu kutakuwa na filamu ambazo zitapigiwa kura na watazamaji wa chaneli ya sinema zetu.