Rose Muhando: Wanaume hunikimbia, sitamani kuolewa

Muktasari:

Mwanamuziki wa nyimbo za injili Rose Muhando amesema hatamani kuolewa kwa sababu kumbukumbu ya kuachwa na muda mfupi baada ya kuanza mahusiano haijamtoka.

Dar es Salaam. Mwanamuziki wa nyimbo za injili nchini Tanzania, Rose Muhando amesema hatamani kuolewa kwa sababu kumbukumbu ya kuachwa na wanaume watatu tofauti muda mfupi baada ya kuanza uhusiano haijamtoka.

Amesema hiyo ndio sababu watoto wake watatu kila mmoja ana baba yake, kusisitiza kuwa wanaume humuacha akiwa mjamzito au na mtoto mdogo.

Akizungumza katika mahojiano na tovuti ya Tuko Kenya, Rose aliyetamba na wimbo wa Nibebe amesema, “sina  mpango wa kuolewa tena, ninabaki na watoto wangu ambao wote wanasoma, sababu kubwa ni kuwa wanaume huniacha muda mfupi baada ya kuanza mahusiano, sioni kama kuna atakayekuwa na tabia tofauti na hawa watatu niliozaa nao.”

Muhando pia alizungumzia sakata la kuanguka kanisani mwaka juzi, kumtaja mchungaji James Ng’ang’a wa kanisa la Neno Evangelism Center la jijini Nairobi kwa kumwita mbele ya kanisa kumuombea wakati akijua kuwa hakuwa na nguvu za kusimama.

Mwaka 2018 zilizagaa video mitandaoni zikimuonyesha Rose mwenye miaka 45  akigalagala kwa maumivu huku akiombewa na mchungaji huyo.

“Sikumbuki ilikuwaje nikaanguka, ninachokumbuka ni kuingia kanisani na  kusikia maneno matatu ya mwanzo ya mchungaji Ng’ang’a akiniombea, baada ya hapo sikujua kilichoendelea  hadi nilipoona video mitandaoni.”

“Mchungaji Ng’ang’a alijua hali yangu siwezi hata kusimama nashangaa kwa nini aliniita tukaombe pamoja, “ amesema.